SERIKALI imetoa zaidi ya Sh bilioni 1 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa shule mbili za sekondari na msingi katika kata ya Mtongani, wilayani Kibaha vijiji, mkoani Pwani.
Hayo yalibainishwa na diwani wa kata ya Mtongani Habiba Hassani, wakati akizungumza na waandishi wa habari, wilayani humo, ambapo alisema serikali imetoa fedha hizo ili kutatua changamoto ya ukosefu wa shule katika kata hiyo.
Alisema serikali imetoa jumla ya Sh milioni 475 kwa ajili ya ujenzi wa shule moja ya msingi na shilingi milioni 528 kwa shule ya sekondari ambapo ujenzi huo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka huu.
“Miaka nenda rudi eneo hili tulikuwa hatuna shule ya msingi Wala sekondari wanafunzi walikuwa wakienda kusoma mbali kwa gharama kubwa hivyo hatua ya serikali ya kutoa pesa za ujenzi huu itatusaidia san.”alisema
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa shule ya msingi Mtongani, Hassan Kazimito Dunia, alisema shule ya hiyo itakuwa na madarasa 16, jengo la utawala Pamoja na vyoo.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Mtongani, Dunia Aliphan akizungumzia ujenzi wa shule ya sekondari, alisema itakuwa na madarasa nane, maabara tatu za masomo ya sayansi, jengo moja la utawa, jengo la tehama na vyoo.
Alisema ujenzi wa shule hizo itaisaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi katika shule ya msingi wa Mtongani ambapo inajumla ya wanafunzi 2,500 na shule ya msingi aAzimio yenye wanafunzi 1,800
“Shule hizi zitasaidia kupunguza mrundikano wa wanafunzi madarasani na itaisaidia sasa watoto wetu kusoma vizuri na kumaliza masomo yao maana wengi wao walikuwa wakishindwa kuendelea na masomo kutokana na gharama na wengine kupata ujauzito kutokana na vishawishi”alisema
Kwa upande wake Katibu wa ofisi ya mbunge wa jimbo la Kibaha Vijijini, Nyamchele Masatu alitoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanawaleta wanafunzi shuleni ikiwemo walemavu na kuacha kuwaficha majumbani.
Akizungumza mmoja wa wananchi wa eneo hilo, Mwanahamisi Kibwana, aliishukuru serikali Kwa hatua hiyo ambapo alisema ujenzi huo utawasaidia kupunguza gharama kutokana na kwamba kila mzazi hutumia kiasi cha Sh 3,000 hadi 4,000 Kwa ajili ya usafiri wa kila siku wa kwenda na kurudi shuleni mwanafunzi.