Sh bilioni 102 kujenga makao makuu MJNUAT

SERIKALI imetenga Sh bilioni 102 kwa ajili ya ujenzi wa Makao Makuu ya Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MJNUAT) cha Butiama kitakachojengwa  kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) ikiwa ni njia ya kuenzi maono ya Nyerere kuhusu utoaji wa elimu ujuzi na elimu ya kilimo.

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,  Profesa  Carolyne Nombo alisema hayo Juni 9, 2023 katika hotuba yake baada ya kushuhudia utiaji saini wa hati ya mikataba miwili ya ushirikiano baina ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na Chuo Kikuu cha MJNUAT kwenye halfa iliyofanyika Kampasi Kuu ya Edward Moringe mkoani Morogoro.

Prof Nombo alisema serikali ipo tayari kuanza kutoa mafunzo katika chuo hicho katika sekta ya kilimo  na Waziri  Profesa Adolf Mkenda alishatoa maelekezo chuo  kianze kutoa mafunzo ambayo yatajikita kwenye kilimo kwa upana wake ambao ulikuwa ni msingi wa uanzishwaji wa chuo hicho na kwamba  kijizatiti kufanya udahili  mwaka wa masomo utakaoanza Novemba 2023.

Katika kutekeleza jukumu hilo alisema, Wizara imetoa Sh bilioni 2.6 kwa Chuo Kikuu hicho  kwa ajili ya kuboresha mazingira  na miundombinu ya kujifunzia na kufundishia ukiwemo ukarabati wa majengo yaliyopo na ujenzi wa  hosteli mbili mpya kwa ajili ya wanafunzi watakaodahiliwa mwaka huu wa masomo.

“ Niwaombe MJNUAT ya kwamba  fedha mlizonazo  mzitumie kwa uaminifu  ili tupate samani  na kuhakikisha kuwa utarabati huu unakamilika kwa wakati ili udahili uliopangwa kufanyika ufanyike  mapema na serikali itaendelea kuongeza wanataaluma  na watumishi wa kada zingine ili kukifanya chuo hiki kitekeleze majukumu yake vizuri” alisema Profesa Nombo

Profesa Nombo alisema maelekezo ya waziri  pamoja na utiaji saini wa Hati za mikataba ya makubaliano yanakifanya Chuo  hicho kuweza kujidhatiti ikiwa ni sehemu ya kufikia vigezo vya kutoa elimu bora ili vijana wa kitanzania wapate fursa ya kusoma katika chuo hicho.

Hivyo aliutaka Uongozi wa MJNUAT kuendelea na mchakato wa kukamilisha mitaala yao na kupata Ithibati kutoka Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), kwani makubaliano yaliyofanyika ya kubadilishana mitaala na wataalamu ( wahadhiri ) ni kukiwezesha kuanza kutoa mafunzo kwa mwaka wa Masomo wa Novemba mwaka huu .

Profesa Nombo alikitaka Chuo Kikuu hicho  kuendelea kukamilisha mitaaa yao waliyoanza kuiandaa na kuhakikisha  zenye Ithibati  ya TCU ambazo zipo chini yao  kwa ajili ya kusaidia kuongeza ubora na udahili wa wanafunzi katika nyanja hizo.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo alisema kwa mwaka wa masomo 2023/2024 serikali imepanga kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu ya juu nchini kwa kudahili wanafunzi wapatao 133,000 kwa mwaka wa kwanza.

Profesa Nombo alisema kuwa, wanafunzi hao wanaotarajiwa kujiunga katika programu mbalimbali  katika ngazi ya Astashahada, Stashahada na Shahada za kwanza .

Makamu Mkuu wa  SUA, Profesa  Raphael Chibunda alisema licha ya  changamoto walizopitia kuandaa mtaala , Chuo hicho  ipo tayari kushirikiana na Chuo Kikuu cha MJNUAT cha Butiama kwa hali na mali na  kutoa mchango wake kusaidia chuo hicho kianze kwani tayari wao ni washirika wa muda mrefu na wala hawashindani zaidi bali ni kuongeza  fursa kwa vijana wa kitanzania kupata elimu ya juu ya chuo kikuu.

“ Tulishafanya hayakwa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MOCU) zaidi ya miaka kumi na mwaka 2023 tunategemea  kuanzisha Shahada ya pamoja” alisema Profesa Chibunda

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo cha MJNUAT , Profesa Lesakit Mellau alisema  kuwa uamuzi wa makubaliano kati ya SUA na Chuo chake  ni wa manufaa kwa nchi yetu  na kutokana na uwezeshaji wa fedha na  Serikali yatari  Chuo kimeanza kufanya  ukarabati wa miundombinu iliyoko ili kukiwezesha kufanya udahili ifikapo Novemba  2023.

Profesa Mellau alisema kupitia fedha zilizotengwa kwa Chuo hicho chini ya  Mradi HEET , zitatumika  kitajenga Ndaki ya Kilimo, Shule Kuu ya Uhandisi Kilimo na Teknolojia ya Umwagiliaji, Shule Kuu ya Uandisi na Teknolojia ya Uchimbaji Madini na Nishati mbadala pamoja Shule Kuu ya TEHAMA na Biashara itayojengwa  Kampasi ya Tabora na kufanya chuo kuweza kudahili wanafunzi 6,200.

Habari Zifananazo

Back to top button