Sh bilioni 16 zahitajika mafunzo kwa wahandisi

BODI ya Usajili wa Wahandisi Tanzania (ERB) imesema ina uhitaji wa Sh bilioni 16 kwa ajili ya kuwezesha mpango wa mafunzo kwa vitendo kwa wahandisi wahitimu (Seap) kwenda vizuri na hivyo, kuomba serikali iwasaidie kupata chanzo endelevu.

Akizungumza Dar es Salaam wakati akifunga mafunzo kwa wahandisi, msajili wa ERB mhandisi Bernad Kavishe alisema kati ya fedha hizo Sh bilioni 3 ni kwa ajili ya ujenzi wa shule ya wahandisi ya mtandaoni.

Aidha Sh bilioni 3 nyingine alisema ni kwa ajili ya vijana ambao tayari wako kwenye mafunzo lakini hawana ufadhili watahitaji kiwango hicho kila mwezi katika ufadhili.

Kavishe alisema Sh bilioni 10 ni kwa ajili ya kuwasaidia waliopo kwenye mafunzo kwani kuna wengine wapo nyumbani hawajajitokeza kwasababu kwa mwaka wahandisi wapya wanaomaliza shule Tanzania na wengine wanatoka nje ni takribani 3500.

“Kwa hiyo kwasababu ni mpango wa miaka mitatu tunaongelea wahandisi 10500. Wale kuwatunza kwa mwezi mmoja ni sh bilioni 10 kwa hiyo bilioni 120 kwa mwaka. Mpango huu tungefanya asilimia 100 wasaidizi wangetupeleka mbali sana kwenye kuongeza kiwango cha wahandisi,”alisema.

Alisema kiwango hicho cha fedha kingerudi baadaye kwa kuwa vijana hao wangewarudisha kwenye jamii na kwenye maeneo ya kazi, wangefanya kazi kwa weledi.

“Tunaomba serikali itusaidie tupate chanzo endelevu cha kusaidia hawa vijana ili mpango wa Seap usiwe wa hiari bali uwe wa lazima kama ilivyo katika fani ya udaktari,”aliongeza.

Alisema tangu mpango huo uanze mwaka 2003 huu ni mwaka wa 21 na tayari wamewanoa na kuwapitisha wahandisi 12000.

Kupitia mpango huo alisema wameanzisha miradi miwili kuna ambao walipewa msaada na serikali ya Norway ambao unanufaisha serikali zote mbili Zanzibar na Tanzania bara na Chama cha Wanawake Wahandisi waliopewa majukumu ya msaada huo kwa ajili ya kuendeleza masomo ya sayansi.

“Tumefanya mafunzo kwa wanufaika karibu watu 500 walioko kwenye mradi na ambao hawapo na kuna waliodandia. Ilikuwa ni muda wetu wa kushukuru wadau na kuwaomba tena wengine waendelee kutusaidia,”alisema.

Rais wa Taasisi ya Wahandisi Tanzania Dk Gemma Modu aliwapongeza washiriki na kuwaasa kuzingatia mambo muhimu waliyofundishwa kwenda kuyatumia katika kujenga msingi imara wa safari yao ya kuwa wahandisi bora wenye ujuzi.

“Muende mkadumishe tabia njema, kufuata maadili ya kitaalam kwenye mambo muhimu ya safari hii ya kuelekea kuwa wahandisi wenye weledi. Mkijitahidi mtasaidia kuongeza kiwango kinachohitajika cha nchi,”alisema.

Miongoni mwa wanufaika wa mpango huo tangu 2018-2021 ambaye ni Mhadhiri Msaidizi katika Chuo cha Maji Mhandisi Nancy Mduma alisema alitoka akiwa mshindani kiasi kwamba anaweza kufanya kazi katika miradi mikubwa nje ya nchi.

Habari Zifananazo

Back to top button