Sh bilioni 17.05 zatolewa mikopo sekta ya mifugo, uvuvi

WIZARA ya Mifugo na Uvuvi imesema kwa mwaka wa fedha 2022/2023 jumla ya Sh bilioni 17.05 zilitolewa mkopo kwenye Sekta za Mifugo na Uvuvi, kupitia Benki ya Maendeleo na Kilimo.

Kati ya fedha hizo Sh bilioni 13.70 zilitolewa kwa wazalishaji katika sekta ya mifugo na Sh bilioni 3.35 zilitolewa kwenye sekta ya uvuvi.

Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema mikopo iliyotolewa Sh bilioni 9.96 ilielekezwa kwenye ufugaji wa kuku, Sh milioni 996.5 ilitolewa kwenye miradi 13 ya unenepeshaji wa ng’ombe iliyopo katika mikoa ya Tabora, Pwani, na 124 Manyara.

Akizungumza bungeni jijini Dodoma, Ulega amesema Sh bilioni 1.31 ilielekezwa kwenye ununuzi wa mitamba 243 na ujenzi wa mabanda ya kisasa ya ng’ombe na Sh milioni 397.70 ilielekezwa kwenye miradi saba ya ufugaji wa Nguruwe iliyopo katika mikoa ya Pwani na Mara.

Amesema Sh milioni 469.89 zilielekezwa kwenye uzalishaji wa chanjo za mifugo na Sh milioni 195.70 ilienda kwenye mradi 1 wa ufugaji wa samaki katika mabwawa uliopo mkoani Pwani.

Aidha, Sh milioni 55 zilitolewa kwenye miradi miwili ya ununuzi na uuzaji wa samaki kutoka Ziwa Victoria iliyopo Ukerewe. Sh bilioni 2.80 zimeelekezwa kwenye miradi miwili ya ufugaji wa samaki kwenye vizimba katika Mkoa wa Mara.

Habari Zifananazo

Back to top button