SERIKALI imetenga Sh bilioni 17.1 kwa ajili ya ukarabati wa hospitali 19 kongwe za wilaya katika mwaka wa fedha 2022/2023.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dk Festo amesema hadi kufikia mwezi Februari mwaka huu, Sh bilioni 12.95 zilikuwa zimekwishatolewa kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa miundombinu katika hospitali kongwe 14.
Dk Dugange amesema hayo leo Aprili 11, 2023 bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Lucy Sabu aliyetaka kujua mpango wa serikali wa kuifanyia ukarabati miundombinu ya Hospitali ya Mji wa Bariadi.
Amesema Serikali imeendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ukarabati wa hospitali kongwe nchini ikwemo ile ya Mji wa Bariadi, ambapo hospitali hiyo imepelekewa Sh milioni 900 na kazi za ujenzi zinaendelea.