Sh bilioni 2 kuboresha huduma ukaguzi TPHPA

MAMLAKA ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), imekabidhiwa vifaa vyenye thamani ya Sh bilioni 2.2 lengo likiwa ni kuhakikisha huduma bora za ukaguzi na uthibiti zinapatikana.

Naibu Waziri wa Kilimo, Dk David Silinde amehudhuria hafla hiyo ya makabidhiano ya vitendea kazi hivyo vilivyotolewa na Shirika la Chakula Duniani ( FAO) pamoja na Umoja wa Ulaya.

Waziri Silinde ametaja vifaa hivyo kuwa ni vifaa vya ukaguzi vya maabara na vya mipakani, vifaa vya kisasa vya uchunguzi na savei za visumbufu

Advertisement

Pia mifumo iliyoboreshwa ya utoaji vibali kwa njia ya kieletroniki na mfumo wa taarifa za maabara.

” Vifaa hivi sio tu, vitasaidia kuimarisha utoaji wa huduma muhimu za mamlaka, lakini pia vitasaidia kuongeza uthibiti na ushindani wa bidhaa za mazao ya kilimo kwenye masoko kikanda na kimataifa,” amesema.

Pia amesema vitendea kazi hivyo vitasaidia kupungua kwa uvamizi wa viisumbufu vipya kutokana na kuimarika kwa soroveya ( survey) ya visumbufu.

Awali Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Profesa Joseph Ndunguru amesema wameshuhudia tukio muhimu la makabidhiano ya vitendea kazi vilivyonunuliwa na FAO.

” Vifaa hivi ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa kuimarisha huduma za afya ya mimea kwa usalama wa chakula Tanzania,” amesema.

Ametaja vifaa hivyo kuwa ni magari saba aina ya Land Crusers, pikipiki 19, ndege nyuki 20, vishikwambi 41, vifaa vya maabara 17, friji 17 na komputer desktop 34 vyote thamani yake ikiwa sh bilioni 2.2.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa mamlaka hiyo, Profesa Andrew Temu amesema yote yaliyofanyika ni juhudi na uwekezaji mkubwa ambao serikali inaweka kwenye sekta ya kilimo.

Amesema Umoja wa Ulaya umeendelea kuonyesha dhamira yake ya kukuza kilimo endelevu.

Pia FAO imekuwa mstari wa mbele katika juhudi za kimataifa za kupambana na wadudu na magonjwa ya mimea.