Sh bilioni 2 zaingia mfuko wa maafa kwa ajili ya Hanang

SERIKALI imesema hadi sasa Sh bilioni 2.7 imeingia kwenye mfuko wa taifa wa maafa kwa ajili ya kusaidia waathirika wa mafuriko yaliyotokea Desemba 4, 2023 wilayani Hanang mkoani Manyara.

Ripoti hiyo imetolewa leo Januari 5, 2024 na Msemaji wa Serikali Mobhare Matinyi alipozungumza na waandishi wa habari akiwasilisha taarifa ya serikali jijini Dar es Salaam.

“Fedha hizi zikijumlishwa na fedha ambazo rais alipokea kutoka Dubai inafanya jumla ya fedha taslimu zilizopo kwa ajili ya maafa haya kufikia bilioni 5.2.” amesema kiongozi huyo.

Advertisement

Sambamba na hilo, Matinyi amesema kuwa Serikali imepokea misaada ya fedha na vitu mbalimbali vyenye thamani ya Sh bilioni 3.1 kutoka kwa wahisani mbalimbali 443 hata hivyo misaada bado inaendelea kupokelewa.

“Wahisani hawa ni watu binafsi, taasisi, mashirika, makampuni ya umma na binafsi, asasi za ndani na nje ya nchi, taasisi za dini na vilabu vya michezo.” Ameongeza Matinyi.