Sh bilioni 20 kuboresha barabara Geita

SERIKALI imetenga zaidi ya Sh bilioni 20 kupitia Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC) kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya barabara ndani ya Halmashauri ya Mji wa Geita.

Meneja wa Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (TARURA) na Mratibu wa TACTIC Halmashauri ya Mji wa Geita, Mhandisi Makongoro Igungu amebainisha hayo katika hafla ya utiaji saini mkataba wa mradi huo.

Amesema ndani ya mji wa Geita mradi huo utajenga kilomita 17 za barabara kwa kiwango cha lami ya zege na tayari mkandarasi ameshapatikana kwa ajili ya utekelezaji.

Amesema wameingia mkataba na kampuni ya Sichuan Road & Bridge Group Corporation Limited chini ya mkandarasi mshauri M/s Luptan Consultants Limited kwa ushirikiano na SAFI Consultants Limited.

Amebainisha kuwa mkataba wa halmashauri na wakandarasi hao kwenye mradi huo ni wa miezi 15 na utekelezaji unatarajiwa kuanza mapema mwezi Novemba, 2023 na kukamilika mapema mwaka 2025.

Meneja wa TARURA wilaya ya Geita Geita, Mhandisi Bahati Subeya ameongeza kuwa mradi huo unaambatana na uwekaji wa taa pamoja na alama za barabarani ili kuongeza ubora wa miundombinu.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Lee Joshua amekiri mradi huo utakapokamilika utabadilisha taswira ya mji wa Geita kwa kupata miundombinu bora ya barabara kwa eneo kubwa.

Mwakilishi wa Mkandarasi wa Kampuni ya Sichuan Road & Bridge Group Corporation Limited kutoka nchini China, See Bo ameahidi kufanya kazi kwa kuzingatia mashariti na muda wa mkataba.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Geita, Mhandisi Costantine Morandi amesema baraza la madiwani limejipanga kusimamia mradi huo kwani mji wa Geita ni miongoni mwa miji 12 pekee iliyonufaika na TACTIC.

Mkuu wa wilaya ya Geita, Cornely Magembe amewaelekeza wahandisi wa halmashauri na wakandarasi kuhakikisha makubaliano ya mkataba yanazingatiwa ili mradi ukamilike kwa wakati na kiwango stahiki.

Habari Zifananazo

Back to top button