TAASISI ya Uhasibu Tanzania (TIA), imetengewa kiasi cha Sh bilioni 27.3 kutoka kwenye Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), zitakazotumika kuboresha mazingira ya kusomea na kujifunza kwa wanafunzi kwa lengo la kutoa wahitimu watakaoweza kujiajiri na kuajiri wengine kulingana na soko la ajira.
Mratibu wa mradi wa HEET kutoka Taasisi hiyo, Oyombe Simba alisema mjini Morogoro kwenye kikao kazi kilichowakutanisha wadau na watumishi wa Taasisi kupitia mchakato wa kuboresha mitaala itakayoenda na matakwa ya utekelezaji wa mradi huo.
Simba ,alisema katika utekelezaji wa mradi huo kuna maeneo saba ya kutekelezwa ukiwemo ujenzi wa hosteli katika kampasi ya Mwanza , kujenga jengo la taaluma kampasi ya Singida na kuboresha wa mitaala itakayompa zaidi mwanafunzi elimu ujuzi anapomaliza chuo aweza kujiajiri ama kuajiri wengine .
Alisema, mradi huo umejikita katika maeneo saba na moja walo ni kuboresha mitaala ili iendane na soko la ajira kwa lengo la kutoa wahitimu wenye kuweza kujiajiri na kuajiri wenzao
Mratibu huyo wa HEET kutoka Taasisi hiyo alisema kuwa, katika kipengere cha uboreshaji wa mitaala kiasi cha takribani sh milioni 250 kinatarajiwa kutumika.
Simba alisema mchakato wa maboresho ya mitaala imeshaanza kwa kufanya kikao cha kwanza cha wadau kupitia mitaala na kufanya maboresho na kupeana uelewa kwa kile kitakachofanyika.
“Katika mchakato huo kutakuwa na maboresho ya mitaala , kutengeneza mitaala mingine mipya na huu ni mchakato ambao kidogo unachukua muda na tunatarajia kadiri ya miezi sita hadi nane ijayo tutakuwa tumetimiza maboresha mitaala na kuja na mingine ambayo itawezesha kukudhi matakwa ya mradi “ alisema Simba
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Uhasibu anayesimamia Taaluma , Utafiti na Ushauri wa Kitaalam wa TIA , Dk Momole Kasambala alisema kuwa, licha ya kuboresha mitaala , mradi huo una lenga uboreshaji wa mifumo (ICT) na Tehama.
“ Tunataka kuchopeka vitu vingi kwenye mtaala yakiwemo masuala ya mifumo au Tehama ili kila taaluma inayotolewa na Taasisi yetu umwezeshe mwanafunzi kujua kila kitu kitaaluma na mengineyo” alisema Dk Kasambala
Dk Kasambala alisema ,mitaala hiyo itakuwa shirikishi kwa watu wenye ulamavu , wanafunzi wenye kunyonyesha na ikijizngatia kijinsia na itakuwa na viwango vya kimataifa kuwawezesha mwanafunzi kutoka nje ya Tanzania na kujiunga kusoma moja kwa moja kwenye Taasisi hiyo.
“ Lengo kubwa ni kuboresha na kuweka mitaala iwe ni ya kimataifa , ijali wenye mahitaji maalum na ichukue masuala na jinsia na kuhusisha program za chuo kupatikana kwenye mtandao au kuchanganya darasani na kwenye mtandao “ alisema Dk Kasambala
Dk Kasambala alisema ,Taasisi hiyo inapitia na kuandaa mitaala sita ambapo mitatu ni kwa ajili ya wanafunzi wa shahada ya Uzamili na mitatu mingine ni kwa ajili ya wanafunzi wa shahada ya kwanza.
Kwa mujibu wa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia ,Profesa Adolf Mkenda ,Septemba 13, 2022 wakati wa utaji saini makubaliano ya utekelezaji wa mradi huo ambao unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kuwa imetoa mkopo wa masharti nafuu wa fedha takribani Sh trilioni moja kwa ajili ya kuleta mageuzi katika utoaji wa elimu juu nchini.
Mradi wa HEET unakwenda kujenga miundombinu, kununua vifaa wezeshi vya kujifunzia na kusomesha wahadhiri ambapo Vyuo Vikuu vya umma 14, Taasisi Tatu zilizo chini ya Wizara zinazosimamia elimu ya juu na Taasisi Tano zilizo chini ya Wizara ya Fedha watanufaika.