MKURUGENZI wa Jiji la Dar es Salaam, Jomaary Satura amesema katika kipindi cha miaka mitatu halmashauri hiyo imetoa Sh bilioni 27 kwa vikundi 880 hivyo, kuzalisha ajira na kuwawezesha Wananchi kiuchumi.
Amesema kupitia mapato ya ndani imewezesha mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu ya Sh bilioni 17.
Akitoa taarifa hiyo leo, Satura amesema kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam inatarajia kupeleka zaidi ya Sh bilioni 8 hadi tisa kwa ajili ya kuwezesha makundi maalumu.
Sambamba na hilo, amesema kutokana na mikopo hiyo halmashauri imeweza kutengeneza viwanda zaidi ya 30 kati ya hivyo kiwanda cha walemavu cha Dege kinachotengeneza vifaa mbalimbali vya chuma ikiwemo vitanda pamoja na vithibiti mwendo (wheel Chairs) kimeweza kufanya kazi kwa ubora zaidi na kuchangia walemavu kutoonekana wakizurura au kuombaomba mjini kwakua wamepata ajira.
“Vijana wamewezeshwa kwa kupatiwa bajaji zaidi ya 546 zenye thamani ya Shilingi bilioni 1.3 pamoja na vijana walemavu wamepatiwa bajaji 211 na bodaboda 546,” ameeleza.
Aidha, amesema mapato ya halmashauri hiyo yameongezeka kutoka Sh bilioni 62 mwaka 2021 hadi Sh bilioni 89 mwaka huu na kwamba wanatarajia kufikia Sh bilioni 120 iwe mara mbili ya bajeti waliyopanga.