Sh bilioni 30 kujenga hospitali ya moyo

DAR ES SALAAM: JENGO jipya la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) litaanza kujengwa mwishoni mwa mwaka 2023 eneo la Mloganzila, ambapo kiasi cha Sh bilioni 30 kitatumika, ili kupanua huduma zinazotolewa na taasisi hiyo na kutoa nafasi kwa wananchi wengi kupata huduma kwa wakati.

Jengo hilo linalojengwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Watu wa China, litakuwa jengo la pili linalotoa huduma za matibabu ya moyo na litakamilika ndani ya miaka mitatu.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kikao kifupi na wajumbe kutoka Serikali ya Watu wa China, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dk Liggyle Vumilia, ameipongeza JKCI kwa kuendeleza uhusiano na China.

“Nia kubwa ya ugeni huu ni kuendelea kukuza mahusiano yaliyokuwepo kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya China, tunaamini ujio wao utasaidia kuendeleza mahusiano yaliyopo na kuhakikisha Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete inaendelea kukua kwa kuanzisha ujenzi wa jengo la JKCI eneo la Mloganzila,” amesema Dk Vumilia.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Mkurugenzi wa Tiba Dk Tatizo Waane, amesema hadi sasa China imeshatuma wataalamu wake kutembelea eneo litakapojengwa jengo la JKCI eneo la Mloganzila na kufanya upembuzi yakinifu uliosaidia kuainisha mahitaji ya vitu vinavyohitajika kuweza kufanikisha ujenzi uliokusudiwa.

Habari Zifananazo

Back to top button