SUMBAWANGA, Rukwa: MKOA wa Rukwa umefanikiwa kupunguza kero ya maji ambapo jumla ya Sh bilioni 31.8 zimetumika katika mwaka wa fedha 2021/22 hadi 2023/24.
Sh bilioni 29.2 zimetumika kusambaza maji vijijini kupitia Wakala ya Usambazaji Maji na Usafi na Mazingira Vijijini (RUWASA) na kufanikiwa kuongeza upatikanaji wa maji kufikia asilimia 64 huku Sh bilioni 2.6 zikifanya kazi kama hiyo Sumbawanga mjini kupitia Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira mjini Sumbawanga (SUWASA).
Akizungumza katika mkutano wake na Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa huo pamoja na waandishi wa habari, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Makongoro Nyerere amesema fedha hizo zimeongeza upatikanaji wa maji mkoani humo.
“…Fedha hizo zimetekeleza miradi 51 ya maji baada ya kutekelezwa miradi hiyo upatikanaji wa maji vijijini umeongezeka kufikia asilimia 64 mwezi januari 2024,
“maji mijini, jumla ya Sh bilioni mbili na milioni mia sita zimetumika kwa ajili ya kuongeza mtandao wa maji manispaa ya sumbawanga.” Amesema Makongoro
Fedha hizo zimeongeza upatikanaji wa maji Sumbawanga mjini kutoka asilimia 86 mwaka 2020 hadi asilimia 94 mnamo januari 2024.