Sh bilioni 43 kutekeleza mradi wa maji Ziwa Victoria
SERIKALI imetoa Sh bilioni 43 kwa ajili ya mradi wa maji Ziwa Victoria kwenye Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama mkoani Shinyanga huku kata 11 na vijiji 60 vikitarajiwa kunufaika.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Christina Mndeme ametoa taarifa hiyo Septemba 18, 2023 akiwa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Bugera kata ya Ulowa katika halmashauri hiyo.
Mndeme alisema serikali inawajali watu wake na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya uchaguzi 2020/2025 inaeleza kumtua mama ndoo kichwani kwa kumuondolea kero ya ukosefu wa maji.
“Mkoa wa Shinyanga umepokea Sh billioni 100 kuboresha mtandao wa maji kwenye halmashauri zote sita na Sh billioni 43 zinakwenda Halmashauri ya Ushetu ili wananchi wapate maji safi na salama.”alisema RC Mndeme.
Mbunge wa jimbo la Ushetu, Emanuel Cherehani alisema kuna kata 20 na vijiji 112 lakini wananchi wanakabiliwa na ukosefu wa maji, hivyo bajeti mwaka wa fedha 2023/2024 serikali imepanga kuleta fedha hizo na maji ya Ziwa Victoria.
Diwani wa kata hiyo, Gabriela Kimaro alisema kata hiyo kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 kuna idadi ya watu zaidi ya 35,000 na ilifanyika tathimini ya kuchimba visima vinane lakini hawakupata maji.
Baadhi ya wananchi wa kijiji hicho, Mande Shija na Amos Jumanne walisema wanaamka saa nane usiku na kurudi saa moja asubuhi kutafuta maji wakati mwingine wananunua dumu la lita 20 kwa Sh 1000.
Meneja wa Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) Wilaya ya Kahama, Paschal Mnyeti alisema usanifu na tathimini umefanyika na wako kwenye harakati ya kutafuta mzabuni na Januari mwakani mradi utaanza kutekelezwa.