UWANJA wa ndege wa unaojengwa eneo la Ibadakuli mkoani Shinyanga umefikia asilimia 6.5 kwenye ujenzi pamoja na upanuzi huku gharama za ujenzi zikiwa Sh billioni 44.8
Meneja wa Wakala ya Barabara nchini (TANROADS) mkoani Shinyanga Mhandisi Mibara Ndirimbi amesema hayo jana wakati wa ziara ya matembezi katika uwanja huo kwa waandishi wa habari mkoani humo.
Mhandisi Mibara Ndirimbi amesema mpaka sasa utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia asilimia 6.5 huku malengo yakiwa ni kufikia asilimia 9.3 ifikapo mwezi Disemba 2023.
“Mradi huu wa ukarabati wa uwanja wa ndege wa Ibadakuli mjini Shinyanga unatarajia kukamilika ndani ya miezi 18 ambapo ulianza utekelezaji Aprili 04 mwaka huu na ifikapo Oktoba 03 2024 utakuwa umekamilika.
Amesema utekelezaji wa mradi huo unahusisha sehemu mbili za ujenzi ambapo sehemu ya kwanza ya ujenzi itahusisha miundombinu mbalilmbali ikiwemo sehemu ya kupaki na kurukia ndege ‘ran way’ na sehemu ya pili inahusisha ujenzi wa jengo la abiria ‘terminal building’ sambamba na mnara wa kuongozea ndege ‘observation tower’.
“Ukarabati na ujenzi wa uwanja wa ndege wa Ibadakuli mjini Shinyanga katika eneo la kuruka na kutua ndege lenye urefu wa kilomita 2.2 umefikia asilimia 50 kwa kilomita moja kukamilika mpaka sasa” ,ameongeza Mhandisi Ndirimbi.
Mhandisi wa vifaa na ushauri kutoka Kampuni ya SMEC Mhandisi Sosthenes Lweikiza amesema wameanza hatua ya awali ujenzi wa jengo la abiria mara baada ya kuondoa miundo mbinu ya maji na umeme iliyokuwa katika eneo hilo.
Mradi wa Ukarabati na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Shinyanga unaojengwa na Mkandarasi China Hennan International Corperation Group Co. Ltd (CHICO) na unaosimamiwa na wakandarasi kutoka Kampuni ya SMEC International ya nchini Australia.
Mhandisi Lwikiza amesema ujenzi umeanza Aprili 4,2023 na unatarajia kukamilika ifikapo Oktoba 3,2024 (ndani miezi 18) kwa ufadhili wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB).