Sh bilioni 6 kutekeleza miradi ya maendeleo Ushetu

HALMASHAURI ya Ushetu wilayani Kahama mkoani Shinyanga imepokea zaidi ya Sh bilioni 6.5 sawa na asilimia 55 ya bajeti iliyotengwa kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Ofisa Mipango wa Halmashauri hiyo, Shigela Ganja amesema hayo leo kwenye kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani cha robo ya pili ya mwaka ambapo waliokuwa na ajenda ya kupitia mapato na matumizi ya fedha zilizokuwa zimetengwa.

Ganja amesema zaidi ya Sh bilioni 6.5 zimetumika katika utekelezaji wa miradi katika nusu mwaka kuanzia Mwezi Julai hadi Disemba ikiwa mapato ya ndani yalikuwa zaidi ya Sh bilioni 1.1 na ruzuku kutoka Serikali Kuu na wafadhili zaidi ya Sh bilioni 5.4.

Ganja amesema mpaka sasa miradi yote umekamilika iliyokuwa kwenye mipango ambapo matundu 66 ya vyoo yamejengwa kwenye shule za msingi kumi ,ukamilishaji wa jengo la mama na mtoto kituo cha afya Igwamanoni na ujenzi wa sekondari moja kata ya Ulowa.

“Halmashauri ilivuka mwaka 2022/2023 ikiwa na zaidi ya Sh bilioni 1.3 zilizokuwa zimetengwa kwa ajili utekelezaji wa miradi katika sekta mbalimbali”amesema Ganja.

Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Hadija Kabojela amesema kila diwani amepitia mapitio ya bajeti iliyotengwa na kuchakata ili kuhakikisha changamoto iliyokuwepo ya ukamilishaji miradi inatekelezwa na hilo limefanikiwa.

Diwani wa kata ya Kinamapula, Samweli Sharifu amepongeza kwa ukamilishaji wa miradi ya maendeleo na ukusanyaji wa mapato katika nusu mwaka kufikia asilimia 103 na hiyo ilitokea mwaka 2014 na historia kujirudia na ndicho walichokuwa wakikitaka siku zote.

Habari Zifananazo

Back to top button