Sh bilioni 8 kutekeleza miradi ya maji 16 Simiyu

WAKALA wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Simiyu imeingia mikataba yenye thamani ya Sh bilioni 8 na wakandarasi 14 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji 16 mkoani humo.

Mikataba hiyo imesainiwa leo mbele ya Mkuu wa Mkoa huo, Dk Yahaya Nawanda ambapo miradi hiyo itatekelezwa katika Wilaya za Meatu, Busega pamoja na Bariadi.

Akizungumza wakati wa zoezi la kutia saini mikataba hiyo, Meneja wa RUWASA Mkoa, Mhandisi Mariamu Majala amesema kuwa miradi hiyo ikikamilika ujenzi wake itaongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji mkoani humo.

Advertisement

Mhandisi Mariamu amesema kuwa hali ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa mkoa wa Simiyu ni asilimia 71.

0, kutoka asilimia 68.20 mwaka 2022.

“Kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Mkoa wa Simiyu uliidhinisha jumla ya Sh bilioni 31.8 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji 32 kwenye wilaya zote tano, kati ya hiyo miradi 16 ndiyo tunasaini leo,” Alisema Mhandisi Mariamu.

Mkuu wa Mkoa akizungumza mara baada ya zoezi la kutia saini kukamilika, amesema kuwa miradi yote 32 ambayo mkoa umepangiwa kutekeleza ikikamilika hali ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa mkoa itafikia asilimia 81.

Dk Nawanda amemshukuru Rais Samia kwa juhudi zake za kuendelea kutoa fedha za miradi ya maji katika mkoa huo, kwani mbali na fedha za miradi hiyo Rais Samia ametoa kiasi cha Sh bilioni 444 kwa ajili ya kutekeleza mradi mkubwa wa maji wa Ziwa Victoria.