Sh bilioni 9 kuwekezwa kilimo cha mpunga gereza la Kalilankulukulu

SERIKALI imetenga Sh bilioni 9 kwa ajili ya kuanzisha kilimo cha umwagiliaji katika mashamba ya mpunga ya Gereza la Kalilankulukulu lililopo Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi.

Akizungumza leo baada ya kutembelea wakulima mbalimbali, Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu amesema hadi kufikia mwezi Aprili mwaka huu Sh milioni 800 kitakuwa kimeshaingizwa kwa ajili ya kuanza ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji katika eneo hilo lenye ukubwa wa takribani ekari mia tano.

DC Buswelu amemhakikishia Rais Dk Samia Suluhu Hassan kuwa watahakikisha wanasimamia kikamilifu na kwa ukaribu mradi huo kwa kuwa si tu utawanufaisha magereza bali utanufaisha pia wananchi wa Mkoa wa Katavi na Taifa kwa ujumla.

Advertisement

Kwa upande wake Mkuu wa Gereza hilo, SP Bosco Lupala amesema katika msimu huu wa kilimo wamelima ekari 150 za zao la mpunga kwa kutumia nguvu kazi ya wafungwa ambapo wanatarajia kuvuna gunia 1700 mpaka 2000 sawa na tani mbili za mpunga.

SP Lupala amemshukuru Rais kwa kutenga fedha kwa ajili ya kuliendeleza eneo hilo kwani ujio wa mradi huo utawapunguzia changamoto mbalimbali huku wakitarajia uzalishaji kuwa mkubwa zaidi kutokana na zana za kisasa zitakazotumika ukilinganisha na ukubwa wa eneo.

Afisa Kilimo Wilaya ya Tanganyika Philemon Mwita amesema wanaendelea kutoa elimu kwa wakulima ili watumie kanuni bora za kilimo ikiwemo matumizi sahihi ya pembejeo.

Kufuatia mradi huo mkubwa, baadhi ya wananchi wawanaozunguka eneo hilo wamemshukuru Rais kwa kuwakumbuka na wanaamini ni mradi utakaowanufaisha ikiwemo kukabiliana na changamoto ya mvua.

Aidha,Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika akiwa ameambatana na Afisa Kilimo wametembelea wakulima wa mazao mbalimbali ikiwa ni kujionea hali ilivyo baada ya mbolea ya ruzuku iliyotelewa na Serikali kama ilitumika ipasavyo na wamejirisha uzalishaji utakuwa mkubwa kutokana na wakulima kuitumia fursa ya pembejeo ya ruzuku.