Sh Mil 884 kutumika TASAF Buhigwe

HALMASHAURI ya Wilaya Buhigwe mkoani Kigoma, inatarajia kutumia kiasi cha Sh milioni 883.9 kwa ajili ya malipo ya walengwa wa mpango wa  kunusuru kaya masikini, ambao wanafanya kazi kwenye miradi midogo ya kuongeza kipato.

Mratibu wa TASAF Halmashauri ya Wilaya Buhigwe, Japhet Mambuya  alisema hayo akizungumza na timu ya waandishi wa habari wanaofanya ziara kutembelea miradi na kuzungumza na walengwa kwenye halmashauri za mkoa Kigoma.

Mratibu huyo alisema kuwa malipo hayo ambayo yanalipwa kwa walengwa ni kutokana na miradi ya aina tatu iliyoibuliwa na walengwa wenyewe, ambayo ni pamoja na miradi ya barabara na vivuko, uboreshaji vyanzo vya maji na upandaji miti.

Walengwa wa TASAF kijiji cha Mnyegera wilaya Buhigwe wakiwa katika mradi wa uboreshaji wa barabara. (Picha zote na Fadhil Abdallah).

“Katika malipo hayo jumla ya walengwa 5183 watalipwa na wasimamizi ngazi ya jamii 115, ambapo miradi hiyo inatekelezwa kwa miezi sita na walengwa watakuwa wanafanya kazi siku 10 za kila mwezi, na malipo hayo hayahusiani na malipo yale mengine ya kawaida ambayo wamekuwa wakipokea,” alisema Mratibu huyo wa TASAF.

Wakizungumzia utrekelezaji wa miradi hiyo walengwa hao wa mpango wa kunusuru kaya masikini, walisema kuwa wameibua kwenye vikao vyao vya mitaa ambapo miradi imezingatia vipaumbele vya upatikanaji huduma, hivyo wakaona kuboresha barabara na vyanzo vya maji ni miradi ambayo inagusa moja kwa moja maisha ya kila siku ya wananchi hao.

Evarist Ntabiliho kutoka kijiji cha Biharu wilaya ya Buhigwe alisema kuwa malipo yanayotokana na kushiriki kwenye miradi kunaongeza kipato cha walengwa, hivyo kuwawezesha kutumia fedha hizo kuimarisha shughuli za miradi yao binafsi.

Mwenyekiti wa serikali ya Kijiji cha Biharu, Conrad Nzweba alisema kuwa jumla ya vyanzo vitatu vya maji vineboreshwa na barabara mita 300, ambavyo ni chaguo la wananchi baada ya huduma hizo kuwa na changamoto.

 

Habari Zifananazo

Back to top button