HALMASHAURI ya Mji wa Newala mkoani Mtwara imetoa Sh milioni 120 kupitia mapato yake ya ndani kwa ajili ya kujenga madarasa manne ambapo mawili yamekamilika na ofisi ya walimu katika shule ya sekondari Chiunjila Ukanda wa Bonde la Mto Ruvuma.
Kukamilika kwa ujenzi huo kuwaondolea wanafunzi changamoto ya kutembea takribani kilometa 10 kila siku kufuata elimu katika kata za jirani.
Akizungumza Julai 18, 2023 kwenye halmashauri hiyo kwa nyakati tofauti kupitia mikutano mbalimbali ya hadhara, Mbunge wa jimbo la Newala Mjini ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu – Kazi Maalum, George Mkuchika amesema wanafunzi wa eneo hilo hulazimika kupanda mlima kuelekea shuleni
Mikutano hiyo imefanyika katika kata tatu kwenye halmashauri hiyo ikiwemo Nanguruwe, Mkunya pamoja na Mcholi moja lengo likiwa ni pamoja na kuwaeleza wananchi mambo mbalimbali yanayofanywa na serikali ikiwemo utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao.
Aidha, wanafunzi wanaoishi ukanda huo wengi wao hushindwa kumaliza masomo yao kutokana na utoro unaosababishwa na uchovu wa kutembea kila siku kwenda ukanda huo kufata huduma hiyo.
Amesema kufuatia uwepo wa changamoto hiyo kwenye kata hizo serikali imefanya juhudi kubwa kujenga shule hiyo ili wanafunzi hao na wananchi wa maeneo hayo kwa ujumla wanaondokane na adha hiyo inayowakabili kwa mda mrefu.
Mwenyekiti wa kijiji cha Chihanga kata ya Mkunya kwenye halmashauri hiyo, Fakihi Mussa amesema mradi wa ujenzi huo unaenda kuwa mkombozi mkubwa kwa wanafunzi wa ukanda wao huo kwani utarahisisha kupata elimu hiyo kwa karibu na urahisi zaidi.
“Kukamilika kwa ujenzi huu kutasaidia watoto wetu sasa hivi kutovuka mlima huu mkubwa kufata shule, kwahiyo kupitia ujenzi huu watapata elimu kwenye mazingira mazuri hapa hapa kwetu kwahiyo tunaishuru na kuipongeza sana serikali yetu kwa kutuletea mradi huu.”amesema Mussa.
Mkazi wa kijiji cha mapili kata ya Nanguruwe kwenye halmashauri hiyo, Hadija Mohamedi “Mpaka sasa tuna matumaini makubwa kukamilika kwa ujenzi huo kwani suala la watoto kukatisha masomo kutokana na changamoto hii litabaki historia tu kwetu na kama wazazi tutahakikisha watoto hawawi watoro tena watasoma kwasababu changamoto ya umbali inaenda kumalizia.”amesema
Ujenzi wa shule hiyo umefikia hatua ya umaliziaji na unatarajia kuanza kuchukua wanafunzi wa kidato cha kwanza Januari 2024.