Akili bandia kutatua magonjwa ya mimea

KIASI cha Sh milioni 150 kimetolewa kwa ajili ya mradi wa mfumo wa akili bandia ‘artificial intelegence’ ili kufuatilia, kutabiri na kupendekeza njia bora za kukabiliana na magonjwa yanayosumbua mimea.

Msimamizi wa mradi wa akili bandia kwa afya ya mmea, Dk Michael Mahenge kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) amesema hayo wakati wa mafunzo ya mfumo huo wa yaliyotolewa kwa baadhi ya wakulima wilayani Mkuranga mkoani Pwani.

Advertisement

Dk Mahenge amesema mfumo huo unatengenezwa kwa kushirikiana na Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), pamoja na shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na utafiti, ushauri wa kitaalamu na miradi ya maendeleo na jamii (Recoda).

Amesema lengo la mradi huo ni kutatua changamoto za magonjwa ya mimea kwa  kutumia teknolojia mbalimbali zikiwemo za akili bandia.

“Upatatikanaji wa taarifa ni picha  za majani ya mimea ili kuweza kuzitafsiri kupitia akili bandia ili kupata taarifa sahihi zitakazomsaidia mkulima hasa katika kukabiliana na mazao hayo.

“Nitumia teknolojia ya ndege zisizotumia rubani, simu janja na kamera za kidijitali katika mashamba ya kuanzia ekari tatu mpaka 100,” amesema.

Ameshukuru serikali kupitia Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech), kwa kuendelea kufadhili miradi katika sekta mbalimbali ikiwemo ya kilimo.

Maelezo yake ni kwamba, teknolojia hiyo itamsaidia mkulima kufuatilia afya ya mmea tangu wakati wa kupanda mpaka kuvuna kwa kumwezesha namna ya kukusanya taarifa shambani.

Amesema mfumo huo unalenga mazao ya kimkakati yanayotumika kwa kilimo yakiwemo maharage, mpunga, mahindi na muhogo ambapo kwa wilaya hiyo ya Mkuranga wanaangalia taarifa za zao la muhogo na mahindi.

Naye Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Kuendeleza Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (Mtusate) kutoka Costech,  Dk Beatrice Lyimo  amesema wamefadhili miradi saba inayotumia akili bandia ili kutatua changamoto katika afya, kilimo, elimu na masuala ya manunuzi.

Amesema mradi huo ambao unatatua changamoto ya afya ya mmea ni moja kati ya miradi saba iliofadhiliwa na tume hiyo kwa kushirikiana na shirika la Maendeleo na Utafiti Canada.

2 comments

Comments are closed.