Sh milioni 240 kusaidia waathirika wa mafuriko Hanang
DAR ES SALAAM: UMOJA wa Makampuni ya Mawasiliano nchini (TAMNOA) umemkabidhi msaada wa zaidi ya Sh milioni 240 kwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ili kushirikiana na Serikali kuwasaidia waathirika wa janga la mafuriko na mmomonyoko wa udongo katika eneo la Katesh, Wilaya ya Hanang, Mkoa wa Manyara.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, leo jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa TAMNOA, Philip Besiimire amesema wameguswa na tukio hilo la kuhuzunisha hivyo kwa umoja wao wamekusanya msaada huo ili kuwafariji waathirika.
Naye, Mkuu wa kitengo cha Habari na Mawasiliano Vodacom Tanzania, Annette Kanora amesema msaada huo umejumuisha vifaa mbalimbali ikiwemo magodoro na vifaa vingine ili kuwarudishia furaha waathirika hao.
Akipokea msaada huo, Waziri Nape amesema “Kwa niaba ya Serikali nimepokea huu mchango na niwaahidi kuufikisha eneo husika.
Amesema wizara yake imepeleka timu wilayani Hanang kufanya uratibu wa miundombinu.
“Taarifa iliyotufikia hii leo, maeneo mengi yapo salama, ispokuwa maeneo machache ambayo tumepeleka majenereta kuhakikisha mawasiliano yanarejea.” Amesema Nape.
Aidha, kiongozi huyo ametoa wito kwa taasisi nyingine kuendelea kusaidia waathirika huko Hanang ambao wamekumbwa na mafuriko yaliyoambatana na matope yaliyoikumba wilaya hiyo usiku wa kuamkia Desemba 03, 2023.