Sh. Milioni 250 Kutatua shida ya maji Ngara

KAGERA: WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso amewahakikishia Wananchi wa kata ya Murusagamba, Wilaya ya Ngara, mkoani Kagera kuwa Serikali imetoa Sh milioni 250 ili kurejesha huduma ya maji katika mji mdogo wa Murusagamba na huduma hiyo itapatikana ndani ya siku 30 kuanzia sasa .

Itakumbukwa, huu ni utekelezaji wa agizo la Naibu Waziri Mkuu, Dotto Biteko ambaye alifanya ziara katika kijiji Cha Ntanga kilichopo katika kata hiyo na kupokea kilio cha diwani wa kata, Sudi Makubira ambaye amesema kuna hatari ya Wananchi kukimbia eneo hilo kwa ukosefu wa maji, kwani mradi uliosanifiwa kuhudumia Wananchi umepitwa na wakati na hautoi maji katika kata hiyo hivyo Wananchi hutumia saa zaidi ya 8 kutafuta maji kuliko kufanya shughuli nyingine.

Biteko alilazimika kumpigia simu Waziri wa Maji katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Ntanga na Waziri huyo alisema ndani ya siku chache angefika kuangalia ufumbuzi wa kupata maji katika eneo la Mji wa Murusagamba ili wananchi wajikite katika shughuli nyingine kuliko kutumia muda mrefu kutafuta maji, jambo ambalo Waziri wa Maji amelitimiza kwa siku tatu .

Akiwa katika Mji wa Murusagamba Aweso amewahakikishia wananchi kuwa ndani ya siku 30 kupitia kwa Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira (RUWASA) Ngara watapata maji safi na salama huku wananchi wa vijiji vingine vya kata hiyo wakisubiri mradi mkubwa wa Sh milioni 700 unaendelea kutelekezwa na serikali kwa mwaka huu wa fedha 2023/2024.

“Nilipokea simu ya Naibu Waziri Mkuu na mkiwa kwenye mkutano nyote mlinisikia, alitoa agizo Ijumaa na mimi leo nipo hapa ikiwa ni siku tatu zimepita, nataka niwahakikishie kuwa nimekaa na watendaji wa RUWASA, Ngara nao wamenihakikishia kuwa wako tayari kukesha hapa ili ndani ya siku 30 mpate maji hapa hapa katika mji huu unaokuwa na hakutakuwa na tatizo la maji ndani ya siku hizo, lakini na kata nyingine tunaendelea kutatua changamoto ya maji serikali iko kazini,” amesema Aweso

Mbunge wa Jimbo la Ngara, Ndaisaba Ruhoro amesema kuwa wakazi wa kata hiyo, huamka Alfajiri kufuata maji na kurudi nyumbani majira ya saa 08:00 mpaka 09:00 za Alasiri Jambo ambalo limekwamisha shughuli za maendeleo katika familia yao.

Amesema kuwa mradi uliokuwepo zamani ulisanifiwa kwa wakazi 2,000 waliookuwepo katika mji huo, lakini kwa sasa wakazi wanafikia 12,000 huku ofisi kadhaa za kuhudumia Umma na shule za bweni zikiwa zimeongezeka katika maeneo hayo.

Amesema kuwa katika Kituo cha Afya Cha Kata hiyo wanawake wanapaswa kabla ya kujifungua kupeleka dumu tano za maji na ndipo huduma ya kujifungua inatolewa.

Aidha, alimuomba Waziri huyo kutimiza ahadi ya kutoa Sh milioni 200 zilizobaki kwenye ahadi yake ya kutoa Sh milioni 500 katika kuboresha huduma za upatikanaji wa maji Ngara mjini ambapo baadhi ya fedha zimetolewa na Wizara ya Maji na bado Sh milioni 200 hazijatolewa ili Wananchi wa Ngara mjini wapate huduma ya maji kwa saa 24.

Habari Zifananazo

Back to top button