Sh milioni 400 zapeleka Neema Nyang’hwale
GEITA: SERIKALI imetumia kiasi cha Sh milioni 486 kununua vifaa vya kisasa mahususi kwa ajili ya kutolea huduma za afya za kibingwa katika hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale, Dk Nevelin Mwakabuku amebainisha hayo leo katika hafla ya uzinduzi wa zoezi la siku tano la utoaji wa huduma bure za kibingwa kwa makundi yote.
Ametaja miongoni mwa vifaa vilivyonunuliwa ni vifaa vya kusafisha damu, vifaa vya wagonjwa wa dharura, vifaa vya upasuaji, vifaa vya wagonjwa wa moyo na vifaa vya huduma ya kinywa na huduma za macho.
Amesema zoezi la siku tano la huduma za kibingwa limeratibiwa kwa ushirikiano na madaktari bingwa wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato (CZRH) ambapo pia watatoa elimu ya matumizi ya vifaa vya kibingwa.
Amesema katika kuboresha huduma za afya mpaka sasa serikali imejenga vituo vya afya vinne na vituo vingine vinne vinajengwa kwa mwaka huu wa fedha ili kufikisha vituo vya afya nane zahanati 28.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale, Husna Toni amesema zaidi ya Sh bilioni mbili zimetumika kuijenga hospitali ya Wilaya na ilianza kutoa huduma za wagonjwa wa nje Machi mosi, 2021.
Ameeleza maboresho yamefanyika na sasa kuna huduma za kibingwa ikiwemo ya vipimo vidogo na vikubwa, huduma za mionzi, X-ray, ultrasound, uchunguzi wa kifua kikuu na kliniki ya mama na mtoto.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Watoto kutoka CZRH, Dk Gerald Muniko amesema huduma za kibingwa wanayotoa ni sehemu ya huduma mkoba kulenga kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi.