Sh milioni 471 kukarabati kituo cha umeme Singida

SERIKALI imesema katika mwaka wa fedha 2023/2024 imetanga Sh milioni 471 kwa ajili ya matengenezo ya njia njia ya kusafirisha umeme msongo wa kilovoti 33 kutoka kituo kikubwa cha kupoza umeme cha Singida kuelekea Manyoni, Itigi, Mitundu hadi Mwamagembe.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato wakati akijibu swali la Mbunge wa Manyoni Magharibi, Hahaya Massare aliyetaka kujua ni lini serikali itafanyia ukarabati mkubwa njia kuu ya umeme inayotokea kituo kikubwa kuelekea Ikungi, Manyoni, Itigi, Mitundu hadi Mwamayembe.

Akijibu swali hilo Bungeni jijini Dodoma leo Mei 11, 2023 kwa niaba ya Waziri wa Nishati, Januari Makamba, Naibu Waziri, Stephen Byabato amesema mkandarasi wa njia ya Reli ya SGR atakapomaliza ujenzi eneo la Kintinku, TANESCO itaunganisha njia ya umeme kutoka Wilaya ya Bahi kwenda Manyoni, hivyo kuimarisha upatikanaji wa umeme katika maeneo hayo.

Akitoa ufafanuzi wa swali hilo, Byabato amesema Mkoa wa Singida umeunganishwa na Gridi ya Taifa kutoka kituo cha kupoza umeme kilichopo mkoani Dodoma kupitia njia za kusafirisha umeme za msongo wa kilovoti 220 na 400 hadi kituo cha kupoza umeme cha Singida.

Amesema kwa kutumia msongo huo mkubwa, Serikali kulingana na upatikanaji wa fedha imepanga kujenga kituo kikubwa cha kupoza umeme wilayani Manyoni ili kuondoa changamoto za umeme kusafiri umbali mrefu.

Habari Zifananazo

Back to top button