SERIKALI Kuu imetoa Sh milioni 603.8 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya sekondari katika kijiji cha Ngilimba kata ya Ulowa Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama mkoani Shinyanga.
Hatua hiyo itawanusuru wanafunzi kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 10 kuelekea shuleni.
Fedha hizo zimetokana na mradi wa uboreshaji wa shule za sekondari (SEQUIP) ambapo zinakuja kwa awamu huku Mkoa wa Shinyanga ikiwa awamu ya pili.
Hayo yamesemwa jana na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Christina Mndeme alipoweka Jiwe la Msingi katika ujenzi wa shule hiyo inayotarajia kuanza kuchukua wanafunzi mwezi Januari mwakani na ipate maji na nishati ya umeme.
Mndeme alimpongeza Adamu Magazi na familia yake ambao walitoa eneo la ekari 12 kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo nakuwapatia serikali ya kijiji na wazazi wawasomeshe watoto wao.
Diwani wa kata ya Ulowa, Gabriela Kimaro amesema kuna vijiji sita ambapo kulikuwa na shule moja ya sekondari ambapo wanafunzi walilazimika kutumia muda mwingi kwenda shule.
“Kwa sasa kutakuwa na shule mbili kwani shule ya zamani iliyopo imeelemewa na wanafunzi zaidi ya 1000 na serikali imetoa fedha hizo tunaishikuru sana imetuondolea kero kwa wanafunzi.”amesema diwani Kimaro.
Mkuu wa shule ya sekondari ya Ulowa ambaye msimamizi wa ujenzi, Godfrey Msimbe amesema shule imeanza kujengwa mwezi Julai mwaka huu nakukamilika Oktoba. Amesema kuna vyumba vinane vya madarasa, matundu ya vyoo manane, tanki la ardhini ,kichomea taka, maabara ya masomo ya sayansi, jengo la Tehama na utawala.
Msimbe amesema wanatarajia mwakani kuanza na wanafunzi 200 na wanaosomea shule ya sekondari Ulowa wanalazimika kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 10 hivyo itaondoa changamoto hiyo.
Afisa elimu sekondari kutoka Halmashauri ya Ushetu, Emanuel Malima amesema kuna shule 23 za sekondari na hiyo ikikamilika zitafika shule 24 kutokana na jiografia ya eneo lilivyo bado shule zinahitajika kuokoa wanafunzi kutembea umbali mrefu
Comments are closed.