HALMASHAURI ya Mji wa Geita imetenga kiasi cha Sh milioni 796.95 kutoka kwenye mapato ya ndani ili kuboresha huduma ya afya ya dharura kwa wagonjwa wenye uhitaji katika kituo cha afya Nyankumbu.
Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Nyankumbu, Irene Temba amesema hayo mbele ya viongozi wa mbio za mwenge kitaifa mwaka 2023 walipofika kwa ajili ya kutembelea na kukagua mradi huo.
Ameeleza, maboresho hayo yamehusisha upanuzi wa kituo hicho cha afya kwa kuongeza majengo saba muhimu katika utoaji wa huduma za afya za dharura hususani wajawazito.
“Mpaka sasa mradi umetumia kiasi cha Sh milioni 622.56, majengo manne yashamekamilika na majengo matatu yapo hatua ya ukamilishaji na yamekasimiwa kiasi cha Sh milioni 50 kwa mwaka huu wa fedha.
“Uboreshaji wa miundombinu umeenda sambamba na ununuzi wa gari aina ya Toyota Land cruiser lenye namba za usajili SM 14941 kwa thamani ya Sh milioni 174.03 kwa ajili ya wagonjwa.” alisema Irene Temba.
Amefafanua kuwa kiasi cha Sh milioni 109.38 kimetumika kujenga jengo la upasuaji, Sh milioni 158.91 imetumika kujenga jengo la kujifungulia, Sh milioni 86.43 imetumika kujenga jengo la maabara.
Ameongeza, pia jengo la kuhifadhia maiti limegharimu Sh milioni 48.74, jengo la kufulia Sh milioni 26.43, nyumba ya mtumishi Sh milioni 47.54, kichomea taka na kondo na mfumo wa maji taka Sh milioni 145.
Mganga mfawidhi ameweka wazi kituo cha afya cha kata ya Nyankumbu mjini Geita kinahudumia wagonjwa 60 mpaka 100 kwa siku idadi ambayo ni wastani wa wagonjwa 2,000 kwa mwezi.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru mwaka 2023, Abdallah Shaibu Kaimu amepongeza mradi huo huku akiwataka watalaamu na wasimamizi wa mradi huo kuongeza nguvu, weledi na uwajibikaji.
“Wahandisi ongezeni usimamizi, au tafuteni namna bora ya kuhakikisha fedha zinazoletwa kwa maendeleo tunakuwa na utalaamu mzuri ambao utatusaidia katika upatikanaji wa miradi bora.”