Sh milioni 800 zatumika ujenzi sekondari ya wasichana

MGODI wa dhahabu wa Barrick Bulyanhulu uliopo Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama mkoani Shinyanga umetoa zaidi ya Sh millioni 800 kwaajili ya ujenzi wa shule maalumu ya sekondari ya wasichana.

Hayo yalielezwa jana na Kaimu Meneja Mahusiano ya Jamii na Mazingira kutoka mgodi huo, Zuwena Senkondo katika ziara ya kutembelea miradi iliyotekelezwa kwa fedha za huduma kwa jamii (CSR ) kwa kuanzia mwaka 2021/2022 na mwaka 2022/2023.

Senkondo alisema fedha hizo zimetolewa kwa awamu mbili na tayari wamejenga vyumba 12 vya madarasa, bweni lenye kuchukua wanafunzi 80 viti na meza 320, maabara ya masomo ya fizikia, biolojia na kemia pamoja na jengo la utawala.

“Shule hii itaanza mwakani rasmi kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne sababu bado ukamilishaji mdogo,watawekewa uzio na Sh millioni 30 za huduma kwa jamii zimetengwa kwaajili ya kuweka umeme na maji kwenye shule hiyo” alisema Senkondo.

Senkondo alisema ujenzi huo umetumia mafundi wazawa (Local fund) na wasambazaji wa vifaa kutoka kampuni ya GekaHil na kuwapatia vijana ajira kutoka kwenye kata ya Bulyanhulu.

Mwalimu James Mukasa ambaye ni msimamizi wa Ujenzi wa shule hiyo alisema shule imejengwa kwenye kijiji cha Busulwangili ikiwa wanafunzi walikuwa wakilazimika kutembea umbali wa kilomita 15 kufuata shule ya sekondari Bulyanhulu.

“Uwepo wa shule hii ya bweni utasaidia kupunguza msongamano wa shule ya sekondari Bulyanhulu yenye wanafunzi 2700 na wanatarajia mwakani kuchukua wanafunzi wa kike 320 katika shule hii mpya kuanza kidato cha kwanza”alisema Mukasa.

Mukasa alisema wanafunzi kuwa bweni wataondokana na vishawishi vya njiani wanafunzi wa kike kupewa lifti na utoro wa rejareja wakati mwingine kukatisha masomo kutokana na kupata mimba.

Mtendaji wa Kijiji cha Busulwangili Asifiwe Greyshen alisema Kijiji hicho kina wakazi 7000 na kaya 423 ikiwa shule hiyo ilianza kujengwa mwaka 2021 na hakuna michango ya wananchi iliyotumika kwenye ujenzi huo.

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Charles Fussi alisema mgodi huo umekuwa ukitoa fedha za huduma kwa jamii (CSR) kwa kila mwaka Sh billioni 2 kwenye kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo elimu, afya na maji.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x