DODOMA. SERIKALI imesema jumla ya shilingi trilioni 10.69 zimetumika kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa.
Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu Kassum Majaliwa wakati akiwasilisha bungeni hotuba yake kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bungwa mwaka 2024/2025 leo bungeni mjini Dodoma.
“Ujenzi wa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro (Kilomita 300) umefikia asilimia 98.84, Morogoro – Makutupora (Kilomita 422) umefikia asilimia 96.35, Mwanza – Isaka (Kilomita 341) umefikia asilimia 52.69.
“Makutupora – Tabora (Kilomita 371) umefikia asilimia 13.86, Tabora – Isaka (Kilomita 165) umefikia asilimia 5.38 na Tabora – Kigoma (Kilomita 506) umefikia asilimia 1.81,” amesema Waziri Mkuu na kuongeza:
“Kama nyote mlivyoshuhudia, majaribio ya treni hiyo ya mwendo kasi yalifanyika kwa mafanikio makubwa mwezi Februari, 2024. Ni matarajio yetu kuwa huduma ya usafiri na usafirishaji itaanza ifikapo Julai, 2024 kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Dodoma.
“ Aidha, reli hiyo ya kisasa itakapoanza kufanya kazi itarahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa baina ya bandari na sehemu za ndani na nje ya nchi.”