Sh trilioni 6 zanufaisha wajasiriamali milioni 8

KIASI cha Sh trilioni 6.1 zimetolewa mkopo na ruzuku kwa wajasirimali milioni 8.6 ambao wameimarisha shughuli zao za biashara na uwekezaji. Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Beng’i Issa ameeleza.

Ben’gi amesema hayo katika maonesho mifuko na program za uwezeshaji wananchi kiuchumi yanayofanyika mjini Kigoma. Amesema kuwa mikopo hiyo imewezeshwa kupitia programu na mifuko ya uwezeshaji 72 inayosimamiwa na baraza hilo tangu ilipoanza miaka 20 iliyopita.

Alisema kuwa hadi kufikia mwezi Machi mwaka huu, mifuko na programu hizo za uwezeshaji zimewezesha kutolewa kwa mikopo hiyo kwa wajasiriamali hao ambao kati yao wajasiriamali wanawake wakiwa ni milioni 4.7 na wanaume milioni 3.9, ambapo ajira milioni 17.6 zimetengenezwa.

Katibu huyo Mtendaji wa NEEC alisema kuwa serikali imejipambanua katika kutekelezaji mpango wa uwezeshaji wananchi kiuchumi, hivyo uwepo wa mifuko hiyo ni utekelezaji wa mpango huo na kwamba maonesho hayo kufanyika Kigoma kunatekeleza azma ya serikali ya kuufanya mkoa huo kuwa wa kimkakati kiuchumi.

Akizungumza katika maonesho hayo Ofisa Habari na Mawasiliano wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Christina Njovu, alisema kuwa ni jambo muhimu kwa wajasiliamali kusajili majina ya biashara zao na kampuni ziweze kutambulika ndani na nje ya nchi kwa urahisi.

Njovu alisema kuwa BRELA inasajili leseni kundi A ambazo kiasi kikubwa zinahusu wafanyabiashara wanaofanya biashara za kuvuka mpaka hivyo wajasiriamali na wafanyabiashara wa Mkoa Kigoma ambao wako mpakani itawapa nafasi nzuri ya kufanya biashara ya kuvuka mpaka na nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Burundi.

Meneja huyo wa BRELA alisema kuwa katika upatikanaji wa mikopo kwa wafanyabiashara na wajasiriamali wanaovuka mpaka kusajili kampuni na majina ya biashara ni mambo muhimu na kwa sasa usajili huo unafanyika kupitia njia ya mtandao na wajasiriamali wanaweza kujisali mahali popote walipo.

Akifungua maonesho hayo Mkuu wa Mkoa Kigoma, Thobias Andengenye amesema kuwa maonesho ya sita ya mifuko na programu ya uwezeshaji wananchi kiuchumi yanayofanyika mkoani humo yataongeza chachu kwa watu mbalimbali kupata habari na taarifa ambazo zitasaidia kuimarisha shughuli zao za uzalishaji na uwekezaji.

Katika hotuba iliyotolewa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya Kigoma, Salum Kalli mkuu huyo wa mkoa kuwa mifuko hiyo ni muhimu kwa wazalishaji na wawekezaji kupata taarifa za fursa zinazopatikana kwenye mifuko hiyo ikiwemo mikopo na uwezeshaji.

Habari Zifananazo

Back to top button