Shahidi aeleza chanzo Mdee, wenzake 18 kufukuzwa Chadema

MJUMBE wa Bodi ya Wadhamini wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Ahmed Khamis (70) ameieleza mahakama kuwa chama hicho kilifikia uamuzi wa kuwafukuza uanachama Halima Mdee na wenzake 18 kwa sababu walipoitwa kwenye kikao na kamati kuu hawakwenda.

Shahidi huyo alidai hayo jana katika Mahakama Kuu Masjala Kuu, Dar es Salaam mbele ya Jaji Cyprian Mkeha wakati akijibu maswali ya dodoso kutoka kwa mawakili watatu wa wabunge hao wa viti maalumu, kutokana na kiapo kinzani alichokiwasilisha mahakamani hapo.

Mawakili hao ni Ipilinga Panya, Joyce Kilinga na Edson Kilatu, ambapo walimuuliza maswali mbalimbali ambayo yalikuwa yakihusiana na suala la Mdee na wenzake kutopewa nafasi ya kusikilizwa na kisha kufukuzwa uanachama wao.

“Nakumbuka walijiapisha ubunge bila kufuata taratibu za uanachama na Kamati Kuu iliwaita hawakwenda na taarifa hizo zilitufikia kwenye Bodi na alizileta Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la chama chetu,” alidai.

Wakili Panya alikuwa akihoji kuhusu madai ya Mdee na wenzake 18 kuwa hawakupewa haki ya kusikilizwa na Baraza Kuu na Kamati Kuu kwa sababu waliitwa kwa barua na wakajibu kwa barua kwamba wapewe siku saba ili waende kujibu lakini hawakupewa nafasi hiyo.

Khamis alidai kuwa hajui kama waliomba au walipewa hizo siku saba anachojua yeye waliitwa hawakwenda.

“Kwenye chama chetu huwezi kufukuzwa bila kusikilizwa na inawezekana walipoitwa kusikilizwa hawakwenda,” alidai.

Baada ya kudai hayo, Panya alimhoji, “ulishaziona nyaraka zao zinazoonesha kwamba waliitwa ila hawakwenda?”

Khamis alijibu kuwa hakuziona nyaraka hizo.

Panya alihoji tena: “Hebu elezea Agosti Mosi hadi 10, 2022 ulikuwa wapi?”

Khamis alijibu kuwa alikuwepo Dar es Salaam.

Panya alihoji kuwa aliandika barua kwenda kwa Halima Mdee na wenzake na alifuata nini Dar es Salaam kwa sababu yeye anaishi Pemba.

Khamis alidai kuwa alienda mkoani hapo kusaini hati ya kiapo za taarifa baada ya kufafanuliwa na mawakili wa tatu ambao ni Kibatala, Hekima Mwasipu na mwingine ambaye hamkumbuki.

Alidai kuwa hakumbuki hicho kiapo kizani alichokisaini kwa sababu hajakiona toka siku aliyoweka sahihi yake.

Alipooneshwa nyaraka hiyo alidai kuwa umri umeenda maandishi hayaoni vizuri anachokiona ni michoro na anakumbuka kiapo hicho walisaini wanane, kila mmoja kwa wakati wake.

Alidai kuwa hakumbuki kikao kilichowaita Halima Mdee na wenzake kilikuwa cha nini, lini na hajui waliitwa wapi.

Khamis alidai kuwa hawajui wajumbe wa kamati kuu walikuwa wapi, anachojua yeye ili iwe kamati kuu lazima iwe na wajumbe 23 na ili kikao kifanyike lazima wawepo hata nusu ya wajumbe hao.

Alidai kuwa mchakato wa kupata ubunge wa viti maalumu unaanzia ngazi ya wilaya, mkoa, kanda na kamati kuu na Mdee na wenzake walikiuka taratibu zote na kujiapisha kuwa wabunge.

Panya alihoji kuwa chama hicho kimeleta muhtasari wa kikao kazi cha Novemba 7, 2022 kilichokaa na wajumbe wa kamati kuu.

Khamis alidai kuwa hakijui kikao hicho kwa sababu yeye sio mjumbe wa kamati kuu na taarifa za vikao vya kamati kuu huwa zinawafikia kwenye bodi kupitia katibu mkuu wa kamati hiyo.

Alidai kuwa chama chao kina mbunge mmoja wa viti maalumu ambaye ni mwanamke lakini hakumbuki anatokea mkoa gani na jina lake.

Wakili Kilatu alihoji kuwa nani ana jukumu la kufuatilia barua kutoka kwa katibu mkuu na msajili wa vyama vya siasa.

Khamis alidai kuwa kama hajaambiwa na Katibu mkuu afuatilie barua basi hawezi kufuatilia.

Alidai kuwa ni sahihi kwamba ruzuku inayopokea chama hicho inatoka kwa serikali, pia alikiri kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi inamtangaza mtu kuwa mbunge.

Baada ya mawakili hao kumaliza kuuliza maswali, kesi hiyo iliahirishwa hadi leo ambapo jopo hilo litamhoji mjumbe mwingine wa bodi hiyo, Mary Joachim (73).

Mdee na wenzake walifungua shauri hilo namba 36/2022 Julai 22, 2022 wakiomba mahakama hiyo ipitie mchakato na uamuzi wa kuwafukuza uanachama na kisha itoe amri tatu.

Katika shauri hilo, wabunge hao wanaiomba mahakama itengue mchakato na uamuzi wa kuwavua uanachama na pia iwalazimishe Chadema kuwapa haki ya kuwasikiliza.

 

Habari Zifananazo

Back to top button