Shahidi aeleza watuhumiwa dawa za kulevya walivyokamatwa

MKAGUZI Msaidizi wa Kitengo cha Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Inspekta John ameeleza namna walivyowakamata washitakiwa watano wanaokabiliwa na mashitaka ya kukutwa na dawa za kulevya aina ya mirungi yenye uzito wa gramu 936.19.

Akitoa ushahidi wake jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Evodia Kyaruzi huku akiongozwa na Wakili wa Serikali, Monica Ndakidemi alidai mnamo Januari 19, mwaka huu akiwa katika eneo lake la kazi aliletewa taarifa na Afande Monica kwamba saa 12:30 jioni kutakuwa na kazi.

Alidai kuwa ilipofika jioni walikutana ofisini na kupewa maelezo kuwa eneo la Buguruni kuna watu wanajihusisha na dawa za kulevya na kuelekea eneo hilo.

Alidai kuwa walipofika waliizunguka nyumba hiyo kwa ajili ya ulinzi kisha wakampigia simu mjumbe, Mwadadi Ally ili afike eneo la tukio kabla hawajaanza upekuzi.

John alidai kuwa mjumbe alifika na kugonga mlango kwenye nyumba ya washitakiwa, alidai kuwa mshitakiwa Safia ambaye ni mama mwenye nyumba alifungua mlango na walijitambulisha kwake na dhumuni la kufika nyumbani kwake.

“Tulianza upekuzi katika chumba cha mama na watoto wa kike hatukukuta kitu chochote kinachohusiana na dawa za kulevya lakini tulipoingia chumba cha watoto wa kiume chenye vitanda viwili tuliwakuta vijana wanne wamelala,” alidai.

Alidai kuwa walianza kufanya uchunguzi na kufanikiwa kukuta vifurushi sita vya majani mabichi yaliyodhaniwa kuwa dawa za kulevya aina ya mirungi ambavyo kimoja kikiwa chini ya godoro, vitatu ndani ya kiroba kilichokuwa na nguo chafu na vingine viwili vilivyokuwa juu ya dari la chooni.

Alidai kuwa walivipatia lebo kwa ajili ya utambuzi, walichukua simu saba za watuhumiwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi, kisha waliwapeleka washitakiwa Kituo cha Polisi Buguruni kwa ajili ya kuwafungulia kesi na walikabidhi vielelezo hivyo kwa inspekta Msope.

Shahidi alizitambua nyaraka mbalimbali ikiwemo ripoti za ukamataji, pia aliwatambua washitakiwa wote mahakamani hapo kwa kuwataja majina yao ambao ni Safia Ige, Ismail Kara, Juma Hamis, Hussein Ally na Mohamed Jumanne.

Wakati huo huo, Mkemia wa Mamlaka ya Maabara Kuu ya Serikali, Rajab Mohamed alidai kuwa mnamo Januari 23, mwaka huu akiwa eneo lake la kazi alipokea bahasha kutoka Jeshi la Polisi likimtaka kufanya uchunguzi wa vielelezo vilivyokuwa kwenye bahasha ambavyo vinadhaniwa kuwa ni dawa za kulevya.

Alidai kuwa alikagua nyaraka zote za polisi na kuvipa vielelezo usajili kisha akafungua bahasha na kukuta kuna vifurushi sita vyenye lebo a,b,c,d,e na f na kupima uzito wa vielelezo hivyo ambapo alipata jumla ya gramu 936.19, alichukua sampuli za majani ya vielelezo hivyo kwa ajili ya uchunguzi wa maabara.

Mohamed alidai kuwa majibu ya uchunguzi yalionesha kuwa vielelezo vina kemikali ya mimea aina ya mirungi, alivifunga vielelezo vyote na kuandaa ripoti ya uchunguzi na kusaini kisha akavipeleka kwa Mkurugenzi wa maabara kwa ajili ya kuthibitisha kwa kuweka muhuri wa moto.

Shahidi alivitambua vielelezo hivyo na kuomba mahakama ipokee kama ushahidi.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Juni 27, mwaka huu kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x