Shaka aagiza waliopoteza bilioni 1.6/- wasakwe

Katibu wa Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka

KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka ameagiza watumishi waliohusika na upotevu wa Sh bilioni 1.6 katika mradi wa ujenzi wa bwawa la umwagiliaji Kijiji cha Inara Wilaya ya Tabora, watafutwe ili kueleza wapi walikopeleka fedha hizo.

Pia, ametoa maelekezo kwa viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tabora kuandaa ripoti maalumu inayohusu mradi huo uliokwama, kisha ripoti hiyo aipate baada ya kumaliza ziara yake ya Mkoa wa Tabora na kurejea Dodoma.

Shaka alitoa maagizo na maelekezo hayo jana baada ya kufika kwenye mradi wa bwawa la umwagiliaji la Inara lililopo Kata ya Ndevelwa, wilayani Tabora na kushuhudia mradi huo ukisuasua na kushindwa kukamilika huku serikali ikiwa imeshatoa Sh bilioni 1.6 ambazo pia kwa mujibu wa taarifa fedha hizo haziendani na kazi iliyofanyika, hivyo kuibua maswali kwa wananchi.

Advertisement

“Hoja iliyopo hapa ni Sh bilioni 1.6 kupigwa juu kwa juu, naagiza tuwatafute waliopiga hii hela ndio hoja ya msingi. Mkurugenzi watafute wako wapi, hela ndefu hiyo ya serikali wamekula, wanakwenda kujenga mradi ambao hauna kiwango,” alisema.

Alisema iwapo Meya akihitaji kusaidiwa kwenye hilo atasaidiwa kwa njia moja au nyingine kwani waliofanya ubadhirifu huo wamechangia kukwamisha mradi huo.

“Hili la Sh bilioni 1.6 ndugu zangu sisi kama Chama hatuwezi kulifumbia macho, tutalifuatilia mpaka dakika ya mwisho tujue hatua gani zimechukuliwa, Mkurugenzi tunasubiri taarifa hatua gani zimechukuliwa kwa waliohusika na ubadhirifu huu wa fedha nyingi za serikali kujenga mradi ambao uko chini ya kiwango, kujenga mradi ambao hauna tija kwa wananchi,” alisema.

Aliongeza: “Na sasa hivi zinatafutwa fedha nyingine ziletwe tena hapa, hii fedha si ya mjomba bwana, hela hii ya Rais Samia Suluhu Hassan si mali ya sadaka, kama kuna mtu anafikiria hii hela ya serikali ni mali ya sadaka, hii si mali ya sadaka na ndio maana tunaifuatilia.”

Alisisitiza kuwa hakuna hata shilingi moja itakayopotea, kwani chama hicho kilipokuwa kinaomba dhamana kwa wananchi, kiliwaahidi kuwapelekea maendeleo na kazi hiyo inafanywa vizuri. Aliongeza kuwa, wabunge na madiwani wanafanya kazi nzuri, lakini wako baadhi ya watumishi ambao sio waadilifu wanadumaza jitihada hizo, hivyo hawawezi kuwavumilia.

“Hiyo biashara haipo tunataka hii fedha tuambiwe tena tunataka ripoti iliyonyooka, nikienda Dodoma naomba ripoti ya mradi huu na jitihada na hatua ambazo zimechukuliwa. Sasa Serikali ya CCM inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inasimama na ninyi wananchi,” alisema Shaka.

Kuhusu malalamiko ya wananchi ya ugawaji wa maeneo ya kilimo cha umwagiliaji kutokana na mradi huo, Shaka alitumia nafasi hiyo kutoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora kujiridhisha kuhusu ugawaji huo ulivyofanyika.

“Watu wanagombania maeneo lakini kuna watumishi wenu wa halmashauri orodha ninayo wamechukua maeneo hapa, sasa anzeni na hao warudishe kwa wananchi maeneo hayo. Ninayo orodha mkitaka niwasaidie nitawapatia nani kachukua nani hajachukua na miongoni mwao wamekuja wamewakodisha watu.”

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *