MKUU wa wilaya ya Kilosa , mkoani Morogoro, Shaka Hamdu Shaka amesema jukumu kubwa ndani ya wilaya hiyo ni kusimamia ipasavyo dhana ya utawala bora, upatikanaji wa haki kwa wananchi kutoka taasisi za umma za utoaji huduma.
Shaka alisema hayo alipokuwa akijibu maswali na hoja mbalimbali za wananchi wa mji mdogo wa Mikumi kwenye mkutano wa hadhara, wakati wa ziara ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yussuf Masauni.
Alisema dhana ya utawala bora haijasimamiwa ipasavyo ndani ya wilaya hiyo, hivyo kusababisha kutokea malalamiko mengi ya wananchi kuhusu vitendo vya rushwa na upatikanaji wa haki.
“ Nilivyoona ndani ya wilaya hii dhana ya utawala bora haijafanya kazi na haijasimamiwa ipasavyo …ukiangalia malalamiko ya wananchi wengi wanalalamikia pengine rushwa , wanalalamikia haki na wamekuwa na kilio cha muda mrefu bila kupatiwa majibu,” alisema Shaka.
Alisema wamejipanga na wamejipambanua kwa kufanya vikao na watendaji wa kata na vijiji, ambao wameelekezwa kusimamia utawala bora , upatikanaji wa haki kwa wananchi na kujiepusha na rushwa.
“Katika jambo hili hatuta mtazama mtu machoni , tutakuwa wakali , tunataka kuhakikisha ya kwamba dhana ya Rais ya kuimarisha utawala bora katika maeneo yetu ya utawala yanaimarika na kufanya kazi vyema,” alisema Shaka.
“ Wananchi hawajasema , yapo malalamiko ukienda kwenye dawati la jinsia yapo malalamiko kuna rushwa inatolewa kama karanga na kuna majibu ambayo sio mazuri, “ alibainisha.
Shaka alisema maeneo hayo yote yatatazamwa kwa mapana yake, ili kusudi viongozi wa ngazi za chini waweze kusimamia maelekezo na maagizo ya Rais na maelelezo ya matakwa ya kisheria katika utendaji wao wa kazi.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mikumi, Dennis Londo aliiomba serikali kuu kuangalia uwezekano wa kuupandisha hadhi mji mdogo wa Mikumi kuwa halmashauri ya mji, ili kusongeza huduma mbalimbali kwa wananchi badala ya ilivyo sasa kutengemea kila jambo halmashauri ya wilaya ya Kilosa.