KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Shaka Hamdu Shaka, amesema fedha zilizotolewa zaidi ya Sh bilioni 100 kwa ajili ya teknolojia ya gesi asilia katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), zitasaidia kupunguza matumizi ya fedha za kigeni zinazotumika katika mafuta.
Shaka ameyasema hayo leo Agosti 29,2022, jijini Dar es Salaam katika ziara ya kutembelea mradi wa kuunganisha mfumo wa gesi asili katika magari (CNG) katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT).
Shaka pia amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza zaidi ya Sh bilioni 100 kwenye eneo hilo.
Amesema kama zitasimamiwa vyema na waliopewa dhamana, matokeo yake yatakuwa makubwa na tija katika nchi.
“Kwa sasa tupo katika vita ya uchumi hili ni la thamani muhimu kwenye mapambano ya vita vya uchumi, ikisimamiwa vyema na hawa wenye dhamana wakifanya kazi yao vizuri matokeo yake ni makubwa na tija kwenye taifa letu, kwanza kupunguza matumizi makubwa ya mafuta kwenye magari yetu,”amesema Shaka na kuongeza:
“Teknolojia hii itasaidia suala la usafirishaji ,endapo uhamasishaji utafanywa vizuri na wafanyabiashara wa ndani wakahamasishwa na serikali ikajipanga vizuri kwenye kujenga vituo vya kusambaza gesi.”
Shaka amesema jambo la msingi ni kuwa na wataalamu wa kutosha ambao watasimamia kazi hiyo.
“Suala jingine ni kusaidia kupunguza tatizo la ajira kwa vijana, endapo mipango itawekwa ya kuwaandaa vijana kwa kutumia fursa hii, ambayo imeibuliwa na kuwatoa kwenye kilio cha ukosefu wa ajira kwa vijana.
“Huu utaratibu ukiwekwa kupitia mikoa na wilaya, DIT ikajitanua naamini tunaweza kuwasaidia vijana na Watanzania kutumia rasilimali hii ya gesi tuliyonayo,” amesema na kuongeza:
“Uchumi tunao na kama uchumi tunao ni lazima utumike vyema, hii mipango itoke katika vichwa vyetu iende kufanya kazi, ili fursa ziende kwa wengi,” alisema Shaka.
Amesema kumekuwa na jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali ya CCM inayoongozwa na Rais Samia, hasa kwenye uwekezaji wa fedha nyingi kwenye miradi ya maendeleo.
Amesema wanayotekeleza sio matakwa yao ama utashi wao, ni kwamba wanasimamia maelekezo ya CCM kupitia Ilani ya chama ya mwaka 2020/2025
Awali Mkurugenzi Mkuu wa DIT, Prof. Preksedius alisema DIT itaendeleea kuwekeza katika vituo vya umahiri, ili iweze kujitegemea na kuishinda vita ya kiuchumi.
Amsema DIT imejitahidi kujitanua katika masula ya teknolijia na kusimamia kifungu cha 67 (c) cha Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi.