Shaka akerwa na mrajis wa ushirika Tabora

Katibu wa Itikadi na Uenezi (CCM), Shaka Hamdu Shaka akipata maelezo kuhusu karakana ya SIDO Mkoa wa Tabora kutoka kwa Meneja wa SIDO wa mkoa huo, Samuel Neligwa, akiwa katika ziara ya kukagua Uhai wa chama na Utekelezaji wa Ilani ya chaguzi ya CCM ya 2020-2025

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeiagiza serikali kupitia Wizara ya Kilimo kumwondoa haraka Mrajis wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Tabora kwa madai amekuwa chanzo cha kukwamisha jitihada za kuwainua wakulima wa zao la tumbaku.

Aidha, kimeshauri kujengwa kwa kiwanda cha kuchakata tumbaku pamoja na kiwanda cha kutengeneza sigara ndani ya Mkoa wa Tabora ambao umekuwa kinara wa kilimo hicho.

Akizungumza jana na wananchi wa Kijiji na Kata ya Ufuluma Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka (pichani) alisema amepokea malalamiko ya wakulima wa tumbaku kuhusu changamoto ya Mrajis wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Tabora, Geophrey Chiliga.

Advertisement

“Changamoto za bwana huyu imekuwa donda sugu, tumetoka Kaliua analalamikiwa, tumetoka Sikonge analalamikiwa, tumetoka Urambo analalamikiwa, leo tuko Uyui watu wanalia na huyu bwana. Urasimu umekuwa mkubwa sana,” alisema.

Shaka alisema anaielekeza Wizara ya Kilimo kupitia Waziri wa Kilimo kumwondoa mara moja Mrajis wa vyama vya ushirika kwa sababu Tabora ndio inaongoza kwa kilimo cha tumbaku hivyo hawawezi kuona jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan zinakwamishwa na mtu mmoja tu.

Aidha, alisema kwa kuwa Tabora imeongoza uzalishaji tumbaku kutoka kilo milioni 16 mpaka kilo milioni 33, ni rai ya CCM kwa Wizara ya Kilimo kujenga kiwanda cha kuchakata tumbaku mkoani humo.

“Lakini wajenge kiwanda hicho sambamba na kufikiria namna bora ya kujenga kiwanda cha kuzalisha sigara hapa Wilaya ya Uyui au ndani ya mkoa huu wa Tabora,” alisema Shaka.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *