Shaka aponda wasiotaka Muungano

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema si ushujaa kwa chama cha siasa kuwa na shauku ya kuvunja Muungano au viongozi wake kupania kuligawa taifa.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka alisema baadhi ya viongozi wa upinzani kwa muda mrefu wako katika juhudi za kushawishi wananchi waone Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hauna maana.

Shaka alisema hayo jana baada ya kikao cha Kamati Maalumu ya NEC kilichoketi mjini Unguja.

“Wapo watu bila Muungano wasingepewa hata usheha. Kutambulika kwao na sauti zao kusikika kwao ni kuwepo kwa Muungano ambao leo wanaudhihaki na kuona sio lolote wala chochote kutokana na ubinafsi wao wa nafsi,” alisema.

Shaka alisema hata ustawi wa utulivu, amani na umoja katika pande mbili za Muungano unatokana na uimara wa Muungano kwa kuwa nje ya Muungano Tanganyika wala Zanzibar hazitabaki salama.

“Ndani ya Muungano kuna uhuru wa kutosha na watu wakiishi kwa amani. Nje ya Muungano usalama utapeperuka. Utulivu wa ndani na wa kisiasa utakosekana. Tusikubali kukichoma kichaka cha Muungano, tutakosa mahali pa kujihifadhi,” alisema na kuongeza:

“Tuna baadhi ya wanasiasa wetu wako tayari hata kuuza utu wao ili wamtumikie shetani aliye kizani. Watu hao kwa bahati nzuri ni wachache wenye uchu wa madaraka. Wangeungwa mkono na wengi tungalizamishwa au kupigwa bei mnadani.”

Shaka alihimiza wananchi wa Unguja na Pemba waendelee kuwa makini kwa kile alichokiita kutahadhari macho yao ili kulinda umoja usivurugwe.

Alisifu uongozi bora, makini na wenye uthubutu wa Rais Samia Suluhu Hassan na Dk Hussein Mwinyi kusimamia sera za mageuzi ya kiuchumi Tanzania.

 

 

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x