KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka amewataka wana CCM kutopoteza muda kwa malumbano na majibizano kwa kuwa kuna kazi muhimu mbele yao ya kujenga Chama na nchi.
Amesema Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi wameanza vizuri uongozi katika kuwatumikia wananchi, hivyo ni jukumu la wana CCM na Watanzania kwa jumla kuwaunga mkono.
Shaka ameyasema hayo leo Desemba 11, 2022 katika hafla ya mapokezi ya Makamu Mwenyekiti wa CCM (Zanzibar) Dk. Hussein Ali Mwinyi yaliyofanyika katika viwanja vya Afisi Kuu ya CCM Zanzibar (Kisiwandui) na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali.
“Niwaombe wana CCM wenzangu tusipoteze muda wa malumbano, tuna kazi ya kukijenga Chama, tuna kazi ya kuijenga nchi, tuna kazi ya kuijenga Zanzibar hii. Dk. Mwinyi ameanza vizuri jasiri mwongoza njia lazima wafuasi tufuate…bega kwa bega.” Amesema.
Shaka amesema Chama Cha Mapinduzi Zanzibar kipo katika mikono salama chini ya uongozi wa Dk. Mwinyi kwa kuwa ameonyesha uwezo mkubwa wa uongozi na kusimamia maendeleo ya wananchi.