Shaka: Rais Samia anaenzi kwa vitendo maono ya Nyerere

Samia aagiza wahitimu Veta wasaidiwe kujitegemea  

KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, amesema Rais Samia Suluhu Hassan anaenzi kwa vitendo maono ya hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere wakati huu Watanzania wakikumbuka miaka 23 ya kifo chake.

Shaka ameyasema hayo leo Oktoba 13,2022, wakati wa ufunguzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) cha Mkoa wa Kagera katika hafla ambayo imefanyika mjini Bukoba, mgeni rasmi akiwa Rais Samia.

“Naomba niseme neno moja lenye uzito wa hali ya juu, Mheshimiwa Rais leo tukiwa tunashuhudia makabidhiano ya chuo hiki cha kisasa kabisa, wote tunakumbuka na wote tunafahamu kwamba tuko kwenye kumbukizi ya miaka 23 ya kifo cha hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Advertisement

“Ndugu Rais tukikumbuka wosia na tukikumbuka moja ya kumbukumbu muhimu, ambazo tumeachiwa na mwasisi wa taifa hili, ni maono pamoja na misingi baada ya kuasisiwa kwa taifa,” amesema na kuongeza:

“Baada ya uhuru, Mwalimu Julius Nyerere alihimiza, alikuwa na maono na mtazamo kwamba siku moja Tanzania iwe na taasisi au kuwa na vyombo, ambavyo vitawasaidia Watanzania, katika kuwajengea uwezo wa kujiajiri kwa mantiki nzima ya kupambana na umasikini.

Amesema Mwalimu Nyerere katika kitabu chake cha Watu na Maendeleo, alisema ukitaka kuleta maendeleo kwa wananchi washirikishe.

“Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, Chama Cha Mapinduzi kinakupongeza kwa dhati kabisa kwa kuishi kwa vitendo maono na dira ya baba wa taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wakati huu tukiwa katika kumbukizi ya miaka 23,” amesema.

Chuo hicho cha VETA Mkoa wa Kagera kimejengwa katika Kata ya Nyakati, Kijiji Cha Burugo, ambapo ujenzi wake umegharimu sh. bilioni 22.4 kikijengwa kwa msaada wa serikali ya China.