Shaka: Rais Samia hajali itikadi kuleta maendeleo

KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, amesema Rais Samia Suluhu Hassan, ameanza uongozi vizuri kwa kuwaunganisha Watanzania, hivyo vyama vya siasa vya upinzani viungane nae kujenga nchi.

Amesema Rais Samia ameonesha dhamira ya dhati kuwaletea maendeleo Watanzania bila ya kujali itikadi zao, ni vyema akaungwa mkono.

Akitoa salamu za chama  kwa wananchi   mjini Kibondo  katika ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan mkoani Kigoma, Shaka amesema ni vyema vyama vyote vya siasa vikaungana na kujenga nchi.

“Tunawashukuru kwa kuja kuona mambo mazuri, karibuni tuungane pamoja tuijenge nchi yetu, nchi ni moja na taifa ni moja, Rais Samia ameanza vizuri kutuunganisha Watanzania mbali na imani zetu na itikadi zetu, lakini Tanzania ni moja,” amesema.

Shaka amewashukuru viongozi wa vyama rafiki walioshiriki mkutano huo kwa kumuunga mkono Rais Samia na kusema sasa ni wakati wa kuunga mkono juhudi za Rais Samia za kuleta maendeleo.

Awali Shaka, amesema Rais Samia ni mwana CCM kindakindaki na mwanamendeleo thabiti aliyedhamiria kuleta maendeleo ya kweli.

Amesema, Rais Samia ameonesha kwa vitendo uthubutu wa hali ya juu kuleta maendeleo ya kweli kwa wananchi.

“Niwahakikishie wana Kigoma na Watanzania, ajenda ya maendeleo kwa Rais Samia Suluhu Hassan ipo katika mikono salama,” amesema.

Amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kipaumbele chake cha kwanza ni maendeleo na hilo limedhihirishwa na mkataba ambao Rais Samia, wabunge na madiwani walikabidhiwa katika uchaguzi wa 2020.

Habari Zifananazo

Back to top button