‘Shangingi’ Ofisi ya RC lagonga lori JWTZ, laua 3

WATU watatu wamefariki dunia baada ya gari aina ya Toyota Land Cruiser ‘Shangingi’, mali ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro, kugonga lori  la Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kisha kupoteza uelekeo na kuparamia waendesha pikipiki na kusababisha vifo hivyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Fortunatus Musilimu, amesema kuwa ajali hiyo imetokea  alfajiri ya saa 11 Desemba 5, mwaka huu (2022),  eneo la Kihonda, Manispaa ya Morogoro  katika  barabara kuu ya Morogoro – Dodoma.

Musilimu amewataja  waliofariki dunia kutokana na ajali hiyo ni Ashirafu Yusuph (43) dereva wa pikipiki yenye usajili namba MC 367 DFM na abiria wake Faustine Polinali (28)  wakazi wa Kihonda.

Mwingine aliyefariku dunia ni Robison  Mazengo( 25) mkazi wa Mkundi aliyekuwa akiendesha pikipiki yenye namba za usajili MC 450 DDL.

Kwa mujibu wa Kamanda huyo, chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva Abed Namangae (53), mkazi wa Mkundi, Manispaa ya Morogoro aliyekuwa akiendesha gari namba T 514 CAQ, Toyota Land Cruiser mali ya ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.

Amesema  dereva huyo  alikuwa akitokea  eneo la  Mkundi,kuelekea mjini na wakati akijaribu kuyapita magari mengine aliligonga gari la JWTZ  lenye namba za usajili 2032 JW12

Amesema baada ya kuligonga gari hilo la JWTZ, gari lake lilipoteza uelekeo na kwenda kuwagonga watu hao waliokuwa wamebebana kwenye pikipiki na kusababisha vifo vyao.

Amesema  dereva huyo  alikuwa peke yake ndani ya gari hilo na kwa sasa anashikiliwa  na polisi na kwamba atafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.

Naye Ofisa  Habari wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro, Scholastica Ndunga amethibitisha kupokea kwa miili ya watu wawili na majeruhi mmoja, ambaye naye alifariki muda mfupi, wakati akipatiwa matibabu.

Kwa upande wake mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Mkude, amedai kuwa  mmoja wa marehemu hao ni dereva wa daladala.

Mkunde amedai dereva huyo alipanda bodaboda kwa ajili ya kuwahi kuchukua gari lake alilokuwa amelaza katika eneo la  kituo cha mafuta Kihonda.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button