Shangwe la Mashujaa lawatisha Geita

TIMU ya soka ya Geita Gold imewasili mjini Kigoma kwa ajili ya mchezo wake wa Ligi Kuu Tanzania Baradhidi ya wenyeji wao timu ya Mashujaa wa Lake Tanganyika, ikisema kuwa ugeni wa Ligi Kuu wa timu ya Mashujaa siyo ugeni wa uwanjani na hawataidharau mechi hiyo.

Kocha Msaidizi wa timu ya Geita Gold, Abubakar Mngazija amesema kuwa usajili uliofanywa na timu ya Mashujaa ni mkubwa kutokana na kuwa na wachezaji wazoefu wa ligi, hivyo jambo hilo linaondoa dhana kwamba timu hiyo ni ngeni.

Pamoja na hilo alisema kuwa vikosi vya ushangiliaji vya mashabiki wa timu hiyo ndiyo vnawatia kiwewe, wapinzani na wao wanahofu kubwa kuvurugwa na washangiliaji wa timu hiyo.

Abdallah Barres Kocha wa Mashujaa

Kwa upande wake nahodha wa  Geita Gold, Elias Maguli alisema kuwa timu ya Mashujaa ina wachezaji wazoefu wa ligi, ambao wamekuwa wakipambana nao na wanawajua vizuri, hivyo wamejiandaa kwa mbinu na kiakili kuhakikisha wanapata ushindi kwenye mchezo huo hata kama wanacheza ugenini.

Akizungumza kwenye mkutano huo kocha wa timu ya Mashujaa, Abdallah Barres alisema kuwa anaiheshimu timu ya Geita Gold kama timu kubwa yenye uzoefu wa ligi, lakini wamejiandaa kuhakikisha wanapata ushindi kwenye mchezo huo.
Barres alisema kuwa michezo miwili ambayo wamecheza ukiwemo wa mechi ya kirafiki na Inter Stars ya Burundi na mechi ya ufunguzi na Kagera Sugar imempa nafasi ya kuangalia mapungufu ya kiufundi, hivyo watayafanyia kazi na wanaamini wachezaji wako timamu kuhakikisha ushindi unapatikana.

Nahodha wa timu ya Mashujaa, Saidi Makapu amesema kuwa wachezaji wapo tayari kwa ajili ya mechi dhidi ya Geita Gold ili kuendeleza ushindi.

Habari Zifananazo

Back to top button