Sheikh Kiburwa: Tuyaishi mafundisho ya dini
KIGOMA: Sheikh wa Mkoa Kigoma, Hassan Iddi Kiburwa amewaongoza waumini wa kiislam katika sala ya Eid huku akihimiza watu wote kufuata mafundisho ya dini yanayokataza tabia mbaya.
Sheikh Kiburwa amesema hayo katika sala ya Eid El Fitr iliyofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi Ujiji Manispaa ya Kigoma Ujiji iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini ya kiislam.
Akitoa nasaha kwa waumini wa kiislam waliohudhuria ibada hiyo ya Eid El Fitr Shekhe Kiburwa aliwataka waumini hao kuungana na watanzania wote kukemea kwa nguvu na kupinga kwa kauli moja vitendo vinavyokwenda kinyuma na maadili ya dini sambamba na vile vinavyokwenda kinyume na mila na desturi za Mtanznaia.
Amewaomba Watanzania kudumisha umoja,amani na mshikamano huku akiongoza waumini kumuombea dua ya afya njema Rais Samia Suluhu Hassan na wasaidizi wake wote ndani ya serikali .
Akizungumza katika sala hiyo ya Eid El Fitr Mkuu wa wilaya Kigoma,Salum Kali amesema kuwa mwezi mtukufu wa Ramadhani waumini wa dini ya kiislam walikuwa wakifanya matendo mema hivyo kumalizika kwa mfungo huo isiwe sababu ya kurudia matendo maovu.