KAIMU Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam,Walid Alhad Omar ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu,Afya na Malezi kwenye Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam.
Sheikh huyo ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo ndogo za Jumuiya hiyo zilizoundwa kuhakikisha zinasaidia kusukuma malengo ya kusimamia suala la malezi ya vijana mkoani hapo.
Akizungumza Dar es Salaam leo Februari 25,2023 wakati akitangaza Kamati hizo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Dar es Salaam Khadija Ally amesema wameunda kamati ndogo ndogo tano ambazo zitasaidiana na kamati ya uendeshaji kutekeleza majukumu yake.
Amesema Kamati hiyo ya elimu, afya na malezi itakua na jukumu la kusimamia malezi ambayo siku za karibuni kumekua na mmomonyoko mkubwa wa maadili kwa Watoto na vijana wa Mkoa wa Dar es Salaam.
“Malezi Bora ni ajenda yetu ya kitaifa kutokana na uzito huo tumeweka viongozi wa dini na wamekuja na kauli mbiu ya malezi bora kwa mtoto faraja ijayo kwa Mzazi na Taifa.
Kamati hii itaenda kutoa mafunzo elekezi kwa viongozi wa ngazi ya Kata na mitaa na inawalimu ambao wapo mashuleni muda wote ambako wanasimamia malezi na maadili. Amesema
Amesema Kamati hiyo ina viongozi wa kiroho akiwemo Kaimu Sheikh wa Mkoa na Mchungaji hiyo yote ni katika kwenda kusimamia malezi ya kiimani kwenye malezi ya wananchi.
“Kusimamia malezi kwa vijana kuhakikisha wanazingatia malezi yanayoendana na utamaduni wa kitanzania,”amesema
Aidha, ametaja kamati nyingine ni ya Uchumi na Maendeleo ambayo inaongozwa na David Minja.
“Hapa Jumuiya itakuwa inabuni miradi kwa hiyo wanakamati watakuwa wanasimamia kuleta mageuzi tunayokusudia.”Amesema
Amesema kamati nyingine ni ya utamaduni michezo na mazingira na ikiwa na malengo ya kujenga mahusiano mazuri kati ya chama na wanachama wake.
“Tutakuwa na timu za wazazi katika Kata zetu,na mashindano mbalimbali kwa ngazi za wilaya hadi mkoa na tunategemea tukifanya vizuri tutaenda hadi nje ya nchi,” amesema
Kamati nyingine iliundwa ni ya Habari na Mawasiliano ambayo inaongozwa na Dotto Mnyadi na Katibu wake Vicky Kimaro wakati kamati ya nidhamu inaongozwa na Walter Msigwa.
Akizungumza baada ya kupokea barua ya uteuzi huo, Sheikh Walid amesema ameupokea uteuzi huo na kwamba anamuomba Mungu katika kamati aliyochaguliwa apewe nguvu ya kulisimamia kwa kina suala la malezi na ukizingatia nafasi yake ni sheikh ni kuwakataza watu mambo mabaya na kufuata mazuri.
Sheikh huyo ambaye ni Imamu Mkuu wa Msikiti wa Kichangani Magomeni amesema Watanzania wote ni mashahidi mmomonyoko wa maadili na malezi ni wimbo wa Taifa kwa sasa.
Hakuna mji wala nyumba, mkoa au nchi iliyosalimika na malezi kila siku tunaona vitu vipya vinakuja na kwa masikitiko juhudi zinachukuliwa lakini hazijafika panapokusudiwa ,” amesema
.