Sheria kulinda faragha za watu yaanza kutumika

WIZARA ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imetangaza kuwa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Namba 11 ya Mwaka 2022 imeanza kutumika tangu Mei Mosi, mwaka huu.

Waziri wa wizara hiyo, Nape Nnauye ameeleza hayo kupitia notisi ya Aprili 25, mwaka huu kuhusu tarehe ya kuanza kutumika kwa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya Mwaka, 2023.

“Notisi inatolewa kwamba tarehe 1 Mei, 2023 imeteuliwa kuwa tarehe ambayo Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi itaanza kutumika,” alieleza Nape.

Bunge lilitunga sheria hiyo na Novemba 27, mwaka jana Rais Samia Suluhu Hassan aliisaini.

Sheria hiyo inaweka masharti kuhusu misingi ya ulinzi wa taarifa binafsi kwa lengo la kuweka kiwango cha chini cha matakwa ya ukusanyaji na uchakataji wa taarifa binafsi.

Pia aliisaini sheria hiyo kwa ajili ya kuanzisha Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, kuimarisha ulinzi wa taarifa binafsi zinazochakatwa na vyombo vya serikali na vyombo binafsi na masuala mengine yanayohusiana na hayo.

Miongoni mwa mambo yanayosisitizwa kwenye sheria hiyo ni uanzishwaji wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ambayo pamoja na mambo mengine, itakuwa jukumu la kufuatilia utekelezaji wa sheria hiyo kwa wakusanyaji na wachakataji, kusajili wakusanyaji na wachakataji.

Tume hiyo pia itakuwa na jukumu la kupokea, kuchunguza na kushughulikia malalamiko kuhusu madai ya ukiukwaji wa ulinzi wa taarifa binafsi na faragha za watu, kuchunguza na kuchukua hatua dhidi ya jambo lolote ambalo itaona linaathiri ulinzi wa taarifa binafsi na faragha za watu.

Baadhi ya taarifa binafsi zinazolindwa na sheria hiyo ni pamoja na taarifa zinazohusu rangi, asili ya kitaifa au kikabila, dini, umri au hali ya ndoa ya mtu binafsi, elimu, historia ya matibabu, jinai au ajira pamoja na namba yoyote ya utambulisho, alama au namna nyingine maalumu inayomtambulisha mtu binafsi.

Taarifa nyingine binafsi zinazolindwa na sheria hiyo ni anwani, alama za vidole au kundi la damu la mtu binafsi, vinasaba, taarifa inayohusu watoto, makosa na miamala ya kifedha ya mtu binafsi.

Aidha, Kifungu 60(1) cha sheria hiyo, sehemu ya tisa inayohusu masharti mengineyo, pamoja na mambo mengine, kinabainisha kuwa mkusanyaji ambaye bila sababu za msingi, atafichua taarifa binafsi kwa njia yoyote ambayo haiendani na madhumuni ambayo taarifa hiyo imekusanywa anatenda kosa.

Pia Kifungu hicho cha 60(6) (a) (b) kinasema kuwa mtu atakayebainika kutenda kosa chini ya kifungu hicho, atakapotiwa hatiani atawajibika.

“Ikiwa ni mtu binafsi, kulipa faini isiyopungua shilingi laki moja na isiyozidi shilingi milioni ishirini au kifungo kwa kipindi kisichozidi miaka kumi au vyote kwa pamoja; na ikiwa ni kampuni au shirika, kulipa faini isiyopungua shilingi milioni moja na isiyozidi shilingi bilioni tano,” imeeleza sheria hiyo.

Habari Zifananazo

Back to top button