Sheria mpya ya usimamizi wa maafa yafanyiwa kazi

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, George Simbachawene

SERIKALI imeandaa mapendekezo ya kutungwa kwa sheria mpya ya usimamizi wa maafa ili kuweka mfumo wa udhibiti na uratibu wa maafa kwa ajili ya hatua za kuzuia na kupunguza madhara ya majanga, kujiandaa kukabili na kurejesha hali pindi maafa yanapotokea.

Akizungumza mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria jijini Dodoma iliyopokea na kujadili Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, George Simbachawene alisema kutungwa kwa sheria hiyo kutaifuta sheria iliyopo sasa ya mwaka 2015 sura ya 242.

Simbachawene alisema awali masuala ya maafa hayakuwa na mfumo wa kisheria wa uratibu hali ambayo imekuwa ikisababisha mgongano wa majukumu hivyo kutungwa kwa sheria hiyo kutabainisha madaraka, wajibu, maamuzi, utunzaji wa rasilimali na muono unaozingatia taarifa za hali ya hewa.

Advertisement

Pia aliongeza kwamba sababu nyingine ya kutunga sheria mpya ya usimamizi wa maafa ni kuimarisha mfumo wa kiutendaji wakati wa maafa na upatikanaji wa taarifa na takwimu za matukio ya maafa na kuweka mfumo mpya wa kitaasisi unaozingatia mfumo wa kiutawala utakaowezesha ushiriki wa wadau wote muhimu kabla, wakati na baada ya maafa kutokea nchini.

Aidha, alisema utungwaji wa sheria utasaidia kutumia taarifa za hali ya hewa na majanga ambapo kamati zitatakiwa kukutana pamoja na utunzaji wa rasilimali ambazo hutumika kukabili na kurejesha hali pamoja na kuzingatia usalama wa wananchi na mali zao.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Najma Giga aliipongeza ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuendelea kushirikiana na kamati kuhakikisha sheria mpya inatungwa kama hatua ya kuzuia na kukabili maafa ambayo husabababisha athari kubwa.