‘Sheria Serikali Mtandao imeboresha utendaji kazi’

DODOMA: Kupitishwa kwa Sheria ya Mamlaka ya Serikali Mtandao Na.10 ya Mwaka 2019, kumeisaidia serikali kuboresha utendaji kazi wake kupitia matumizi ya teknolojia.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Ridhiwani Kikwete ametoa kauli hiyo bungeni leo Agosti 31,2023 alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Janejelly Ntate, aliyetaka kujua ni lini serikali itarekebisha sheria za utumishi zilizopitwa na wakati hasa kipindi hiki cha teknolojia.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri amesema srikali inatambua uwepo wa maendeleo makubwa ya kiteknolojia, ambayo yamekuwa nyenzo muhimu katika kuimarisha utendaji kazi katika utumishi wa umma.

Advertisement

“Ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia, serikali imeendelea kufanya mapitio ya Mfumo wa Kisheria unaosimamia Utumishi wa Umma, ambapo mwaka 2019 serikali ilitunga Sheria ya Mamlaka ya Serikali Mtandao Na.10 ya Mwaka 2019, ili kuweka mazingira wezeshi ya matumizi ya teknolojia katika utendaji kazi wa Serikali.

“Kupitishwa kwa sheria hiyo kumeisaidia serikali kuboresha utendaji kazi wake kupitia matumizi ya teknolojia.

“Pamoja na mambo mengine sheria hiyo imewezesha kusanifiwa na kujengwa kwa jumla ya mifumo 860 ya TEHAMA serikalini.

“Serikali inaendelea na hatua za kupitia na kufanya marekebisho ya sheria mbalimbali zinazosimamia utumishi wa umma na kanuni zake ili kuhakikisha kwamba zinaendana na mabadiliko ya teknolojia,” amesema.

 

2 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *