Shigella: Nitafuatilia kila senti fedha za miradi

MKUU wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella amesema ofisi yake imejipanga kufuatilia, kupitia na kuweka mikakati thabiti ya usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa wilayani Geita kwa Mfuko wa Fedha za Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR).

Shigella alisema hayo jumanne katika mkutano wake na viongozi wa dini, kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa pamoja na baraza la wazee.

Alisema serikali ilianzisha utaratibu wa kampuni kubwa zinazojihusisha na uchimbaji wa madini kutoa CSR ili kusaidia wananchi kwenye maeneo ya uchimbaji waweze kunufaika hivyo ni lazima matunda yaonekane.

“Mkoa wetu na hasa kwenye halmashauri hizi mbili (halmashauri ya mji na halmashauri ya wilaya ya Geita) wanapata Sh bilioni 9.2 kila mwaka. Ni fedha nyingi sana.

“Tutaweka msukumo kwenye hizi fedha, zilete athari zinazoonekana. Hatuwezi kuwa na shilingi bilioni tisa stendi yetu ikaendelea kuwa ya vumbi.

“Hata kama tunajenga stendi kubwa basi tujenge ile stendi ya sasa iwe ya daladala, iwe ya kisasa zaidi, hatuwezi kuwa na shilingi bilioni tisa tukawa hatuna mitaro ambayo inapitisha maji.

“Wakati mwingine hizi fedha zinaonekana kama siyo fedha za umma, lakini hizi ni fedha za umma. Serikali imetunga sheria, ndio maana tunataka zilete maendeleo kwenye maeneo yetu, kwa hiyo nataka niwahakikishie jambo hili tumelibeba kwa uzito unaostahili,” alisisitiza.

Awali Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Mtaa wa Nyanza Mjini Geita, John Luhemeja aliiomba Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita kufanyia mapitio miradi ya kimkakati inayotekelezwa mkoani hapa ili kujua kikwazo.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button