Shilingi bilioni 1.2 kunufaisha wafugaji
SERIKALI kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imetoa mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 1.2 kwa vikundi vya wafugaji.
Akizungumza leo wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya unywaji maziwa shuleni iliyofanyika katika Viwanja vya Nyerere Square Jijini hapa ,Ofisa Biashara Mkuu wa TADB Daniel Mwalyayo alisema kuwa katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali kupitia Benki hiyo iimeweza kutoa mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 1.2 kwa vikundi 10 vya wafugaji Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kati na Nyanda za Juu Kusini
Alisema kuwa mikopo hiyo imetolewa kwa lengo la kuimarisha ufugaji wa kibiashara wa ng’ombe wa maziwa na kuongeza uzalishaji wa maziwa nchini.
Alisema kuwa wafugaji walikuwa wakipata changamoto ya uzalishaji lakini sasa uzalishaji umeongezeka sasa wanapata hadi lita 30 kwa siku tofauti na awali ambapo ng’ombe walikuwa wakitoa lita mbili hadi saba kwa siku.
Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule alisema kuwa zaidi ya nchi 70 duniani ikiwemo Tanzania zinaadhimisha siku ya unywaji maziwa na tayari zilishaanzisha mpango wa unywaji maziwa shuleni kwa watoto wao.
” Lengo ni kuhakikisha mtoto anapata lishe kamili na anakuwa na usikivu mzuri katika masomo yake.” Amesema
Amesema Mtoto amelengwa kwa sababu ni kundi ambalo ni muhimu katika kujenga Taifa lililo bora na anatarajiwa kurithisha vema vizazi vijavyo.
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni “ Faulu Mtihani kwa Glass Moja ya Maziwa Kila Siku”.
Mpango wa unywaji maziwa shuleni ulianza kutekelezwa mwaka 2007.