SERIKALI imetenga Shilingi Bilioni 23 kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya watoto njiti ili kupunguza vifo kwa watoto hao.
Hayo yamebainishwa leo Septemba 20, 2022 na Naibu Waziri wa Afya Dk. Godwin Mollel kwenye mkutano wa Nane Kikao cha Sita cha Bunge akiwa anajibu swali la nyongeza lililoulizwa na Bunge wa Viti Maalum Cecilia Paraso aliyetaka kujua serikali inampango gani wa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi nchini.
“nikuhakikishie kwamba vifo vitokanavyo na uzazi vimekuwa vikipungua kutokana na juhudi za serikali kujenga vituo vya afya vya dharula kila mahali nchini ili wakina mama waweze kujifungua salama.”
Awali, katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalum Suma Fyandomu alihoji ni lini hospital ya Rufaa Mbeya Meta itaanza kutumika kwa wakinamama wajawazito baada ya kufunguliwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Akijibu swali hilo Dkt. Mollel amesema kuwa vifaa vitakavyotumika katika hospitali ya Rufaa Mbeya Meta vimeshanunuliwa vyenye thamani ya Bil. 2.1 na ndani ya miezi miwili vitafikishwa katika hospitali hiyo na kuanza kutumika.
Aidha Dkt. Mollel amesema juhudi kubwa zimekuwa zikiendelea kuchukuliwa na Serikali kuhakikisha huduma bora za afya zinatolewa nchini kwa kujenga vituo vya afya na hospital za Rufaa nchini.
Pia, amesisitiza kwa kila mama mjamzito ajifungulie katika vituo vya afya au Zahanati ili utambuzi uweze kufanyika na kumpa mtoto tiba stahiki pindi anapogundulika kuwa na tatizo.
Aidha, Dk Mollel amesema serikali imechukua hatua pia kwa Watoto wanaozaliwa na Sikoseli ili kupunguza tatizo hilo kwa kutenga kiasi cha pesa kwa ajili ya dawa ambazo zitasambazwa kwenye vituo vya afya kwa utaratibu maalum.