Shilole atoa ushauri kwa vijana

MSANII wa muziki wa Bongo Fleva, Zuwena Mohamed ‘Shilole’ amewashauri vijana wa kike na kiume kutumia vizuri vipaji vyao ili kuishi maisha ya ndoto zao.

Akizungumza na HabariLEO Jumatano, Shilole alisema kuwa yeye ni mmoja wa watu waliotumia kipaji chake vizuri na maisha yamemnyookea siyo kama alivyokuwa mwanzo.

“Umaarufu niliokuwa nao hivi sasa umetokana na kuthamini kipaji nilichokuwa nacho na kukifanyia kazi, leo namshukuru Mungu maisha yangu ni mazuri namiliki nyumba, usafiri na familia yangu haina shida ndogondogo,” alisema Shilole.

Msanii huyo alisema anaamini vijana wengi wana vipaji vikubwa lakini kinachofanya washindwe kutoka ni kutotekeleza kile ambacho hisia zao zinawatuma kukifanya.

Alisema inawezekana kwa kuhofia aibu na jamii lakini katika mapambano ya maisha hawapaswi kuhofia hilo ndio maana yeye leo amefika hapo alipo kutokana na kuangalia nini nafsi yake inamtuma kufanya na kulingana na kipaji chake.

Shilole mbali ya kuimba muziki lakini pia anamiliki mgahawa mkubwa wa chakula ambao unamwongezea kipato na kuimarisha maisha yake. Amewahi pia kuigiza filamu miaka ya nyuma.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button